Kesi hiyo iliibuka Ijumaa iliyopita wakati shahidi wa 11 upande wa mashtaka, Koplo Seleman Faraji alipotaka kutoa maelezo ya kukiri makosa ya mshtakiwa huyo kama kielelezo.
Mawakili wa utetezi wakiongozwa na Majura Magafu walipinga kutolewa kwa maelezo hayo yaliyochukuliwa na Koplo Seleman Agosti 16, 2013 akisema mshtakiwa aliteswa na polisi.
Wakili Magafu alidai kuwa mteja wake alimweleza kuwa siku hiyo alikuwa hajakamatwa na Agosti 18 aliteswa na kulazimishwa kusaini maelezo ambayo hayafahamu.
Pia, Wakili Magafu alieleza kuwa baada ya mshtakiwa kuteswa na kuumizwa, polisi waliingiwa hofu kuwa angeweza kufa katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi hivyo Agosti 21, 2013 wakampeleka hospitali.
Akitoa ushahidi wake jana katika shauri hilo, koplo Derick alidai kuwa Agosti 18, 2013 majira ya asubuhi akiwa ofisini kwake aliitwa na afande Chiluba akimtaka kumpeleka mshtakiwa mkoani Arusha.
Shahidi huyo akiongozwa na wakili wa Serikali, Omar Kibwana akisaidiana na Abdallah Chavula, Kassim Nassir na Lilian Kyusa, aliieleza mahakama hiyo mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo kuwa lengo la kumpeleka mshtakiwa Arusha lilikuwa ni kuwaonyesha silaha.
Koplo Derick alidai kuwa mshtakiwa alikuwa katika hali nzuri na alifungwa pingu na kwamba wakiwa kwenye gari walipofika eneo la King’ori kulikuwa na foleni na gari lilipunguza mwendo ghafla mshtakiwa aliruka.
Alieleza kuwa baada ya kuruka kwenye gari alianza kukimbia huku akichechemea hivyo polisi waligonga gari kutoa ishara kwa dereva asimame na walianza kumkimbiza na kumkamata.
Koplo Derick alieleza kuwa baada ya kumkamata afande Chilumba alimuamuru dereva kugeuza gari kurudi Moshi na walipofika walimrudisha mahabusu na kuendelea na majukumu mengine.
Baada ya kumaliza kuongozwa na wakili Kibwana, ilikuwa zamu ya mawakili wa utetezi wakiongozwa na Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu.
Wakili Ndusyepo: Agosti 18, 2013 ulipangiwa kazi gani?
Shahidi: Nilikuwa nikifanya shughuli nyingine za ofisi ambazo ni za kipelelezi.
Wakili Ndusyepo: Shaibu umemuona mara ngapi?
Shahidi: Nilimuona siku hiyo nilipomtoa Kilimanjaro kwenda Arusha.
Wakili Ndusyepo: Kitu gani kimekufanya umtambue Shaibu?
Shahidi: Kitendo cha kufanya jaribio la kutaka kutoroka chini ya ulinzi wa polisi ni jambo linalohatarisha kazi yangu.
Wakili Ndusyepo: Je, mlifungua taarifa za mshtakiwa Shaibu kutaka kutoroka chini ya ulinzi wa polisi?
Shahidi: Sikumbuki kwani nilikuwa na kiongozi wangu Inspekta Chilumba.
Wakili Ndusyepo: Unakubali kuwa wewe ni shuhuda wa tukio hilo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Ndusyepo: Uliandika maelezo ya tukio unalolizungumzia?
Shahidi: Sikufungua.
Wakili Ndusyepo: Kwa nini haukuandika?
Shahidi: Kwa sababu sikuwa peke yangu na zaidi ya yote nilikuwa na incharge (msimamizi) wangu Inspekta Chilumba.
Wakili Ndusyepo: Mahakama hii itaamini vipi kulikuwa na jaribio la kutaka kutoroka?
Shahidi: Mlalamikaji ndiye alitakiwa kuandika maelezo.
Baada ya maelezo hayo Wakili Magafu anaanza kumhoji.
Wakili Majura: Shahidi ieleze mahakama hii umesoma hadi darasa la ngapi?
Shahidi: Hadi darasa la saba
Wakili Majura: Shule gani?
Shahidi: Shule ya Msingi Kizuka.
Wakili Majura: Ulijiunga na jeshi lini?
Shahidi: Mwaka 2007.
Wakili Majura: Unaweza kukumbuka Shaibu alikamatwa lini?
Shahidi: Siwezi kwa sababu sikuwapo siku akikamatwa.
Wakili Majura: Wakati mnamchukuwa mlimtoa wapi?
Shahidi:Tulimtoa lockup (mahabusu) ya polisi.
Wakili Majura: Nani alikwenda kumtoa mahabusu?
Shahidi: Mimi na mwenzangu.
Wakili Majura: Unajua mshtakiwa kutoroka chini ya mikono ya polisi ni kosa la jinai?
Shahidi: Sijui.
Wakili Majura: Kwa hiyo ndiyo maana hukuona umuhimu wa kuandika maelezo ya mshtakiwa kuruka kwenye gari la polisi?
Shahidi: Inspekta Chilumba ndiye alipaswa kuandika maelezo.
Wakili Majura: Mshtakiwa alikuwa amekaa upande gani?
Shahidi: Upande wa kushoto karibu na kebini.
Wakili Majura: Unao uzoefu wa miaka mingapi kusindikiza watuhumiwa kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine?
Shahidi: Karibia miaka 11.
Wakili Majura: Uliwahi kusikia kama mtuhumiwa alichukuliwa kwenda kuhojiwa kutokana na tukio alilolifanya la kutoroka?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Majura: Nani alikwambia alihojiwa ?
Shahidi: Inspekta Chilumba.
Wakili Majura: Utakubaliana na mimi hakuna tukio la namna hii lilishawahi kutokea?
Shahidi: Hapana.
Wakili Majura: Lini ulipewa taarifa ya kuja kutoa ushahidi?
Shahidi: Wiki iliyopita.
Wakili Majura: Ulipewa samansi kutoka mahakamani au kwa maneno?
Shahidi: Kwa mdomo.
Wakili Majura: Uliambiwa na nani?
Shahidi: Afande RCO (mkuu wa upelelezi mkoa) Dotto.
Wakili Majura: Alikwambia unakuja kutoa ushahidi kuhusu nini?
Shahidi: Nilijulishwa kuwa nahitajika mahakamani.
Wakili Majura: Nani alikupa taarifa ya kuja kutoa ushahidi wa aliyeruka kwenye gari?
Shahidi: Wakili wa Serikali.
Wakili Majura: Wakili yupi?
Shahidi: Wakili (Abdallah) Chavula.
Wakili Majura: Wakili wa Serikali alijuaje wewe ulikuwa na mshtakiwa kwenye gari?
Shahidi: Sijui yeye alijuaje.
Wakili Majura: Ni kweli hujawahi kuandika statement (maelezo).
Shahidi: Kweli.
Wakili Majura: Nikikwambia ulihusika kumchukua mshtakiwa na kumpeleka kwenye mateso utasemaje?
Shahidi: Siyo mimi.
Wakili Majura: Unasema baada ya kusimamisha gari, mshtakiwa aliruka?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Majura: Na alikuwa ameumia sana?
Shahidi: Alikuwa ameumia ndiyo, aliumia mguuni na kuchubuka sana.
Wakili Majura: Alikuwa anaweza kutembea mwenyewe baada ya kumkamata?
Shahidi: Tulikuwa tunamshikilia na kumuingiza kwenye gari.
Wakili Majura: Je, aliruka umbali gani mpaka mkamkamata?
Shahidi: Kama mita mia moja hivi.
Wakili Majura: Kwenye gari mlikuwa mnajua ni mshtakiwa wa mauaji ya Erasto Msuya, kweli au si kweli?
Shahidi: Kweli.
Wakili Majura: Ulimwadhibu kidogo?
Shahidi: Hakupigwa.
Wakili Majura: Baada ya yeye kuumia, uliwahi kujua alichukuliwa na kupelekwa kwenye matibabu?
Shahidi: Hapana.
Wakili Majura: Kuna mwenzako mlikuwa naye kwenye gari ambaye aliwahi kuhojiwa, ametoa taarifa za mshtakiwa kuruka kwenye gari?
Shahidi: Mimi sijui.
Wakili Majura: Mtu akikamatwa na kupelekwa kituoni na kuwekwa mahabusu, anawekwa kwenye lockup register (rejista ya mahabusu) lazima usaini, wewe ulisaini?
Shahidi: Ndiyo.
Bilionea Msuya aliuawa Agosti 7, 2013 Mijohoroni wilayani Hai, Kilimanjaro. Kesi hiyo inawakabili washtakiwa saba; Shaibu Said, Sadiki Jabir, Karim Kihundwa, Ally Mussa au Majeshi, Jalila Said na Sharifu Athuman.
No comments:
Post a Comment