Thursday, November 2

China ilivyopania kuondokana na umaskini ifikapo mwaka 2020



Moja kati ya changamoto inayozikabili nchi nyingi za Dunia ya tatu ni umaskini. Kumekuwa na njia na mikakati mingi ya kuondokana na jinamizi hili lakini wanaotoka katika mnyororo huo ni wachache mno.
China, taifa linalopiga hatua kubwa na za haraka za maendeleo duniani nayo imekuwa ikikabiliwa na janga hili lakini imekaa chini na kuandaa mkakati kisha kuja na azimio kwamba ifikapo mwaka 2020, kila Mchina aishiye kijijini aliye chini ya mstari wa umaskini anaondoka huko.
Hiyo ni sehemu ya kipengele mojawapo kati ya 13 vya kimkakati vilivyobainishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti China (CPC), Rais Xi Jinping katika Mkutano Mkuu wa 19 wa chama hicho uliomalizika hivi karibu jijini Beijing.
Akizungumzia utendaji wa miaka mitano iliyopita, Rais Jinping aliwaambia wajumbe 2,280 wa mkutano huo kuwa hatua kadhaa za makusudi zimefanywa katika kupambana na umaskini na matokeo yake ni kwamba zaidi ya watu milioni 60 wameondolewa katika lindi hilo, “Pia idadi ya maskini mmojammoja imepungua kutoka asilimia 10.2 hadi kufikia asilimia nne.”
Alisema mafanikio hayo yametokana na maendeleo ya kielimu na ushirikishwaji uliofanywa katika mikoa ya Kati, Magharibi na maeneo ya vijijini.
“Ukuaji wa ajira umeongezeka kwa wastani wa zaidi milioni 13 katika maeneo ya mijini. Kukua kwa kipato cha mtu wa mjini na kijijini kimekua na kipato cha watu wa kati kimeongezeka.”
Jinsi CPC ilivyojipanga kukabiliana na umaskini
Moja ya ahadi zinazotekelezwa kwa umakini mkubwa kwa mujibu wa Rais Jinping ni kuhakikisha kwamba watu maskini na maeneo maskini yanaingia katika maisha bora ya kisasa na kuwa na jamii nzima yenye mafanikio.
“Tutakusanya nguvu za chama chetu chote, nchi nzima, na jamii yetu yote na kuendelea kutekeleza mikakati tuliyojiwekea ya kuondokana na umaskini. Tutaendesha shughuli zetu katika mfumo wa utendaji kazi ambao Serikali Kuu itabuni mipango yote, Serikali ngazi za mikoa zitabeba majukumu yote na Serikali za majiji na miji zitahakikisha kunakuwa na utekelezaji na tutaimarisha mfumo ambako wakuu wa kamati za chama na serikali katika ngazi zote watabeba dhamana ya kuhakikisha tunaondokana na umaskini.”
Kiongozi huyo anasema ili kuhakikisha jukumu hilo linafanikiwa, ushirikishwaji wa pamoja baina ya Serikali, jamii na masoko utaendelea kutiliwa mkazo.
“Tutawasaidia wananchi kuongeza kujiamini kwamba wenyewe wanaweza kuondoka kwenye umaskini na kuhakikisha kwamba wanapata elimu wanayohitaji ili kufanya hivyo.”
Mkakati mwingine anautaja kuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kupambana na umaskini baina ya mikoa ya Mashariki na Magharibi na kutoa kipaumbele katika maeneo ambayo yaliyotopea kwa umasikini.
“Lazima tuhakikishe kwamba ifikapo mwaka 2020, wakazi wote wa vijijini wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa sasa, wanaondoka katika umaskini na umaskini unaondoka katika kata na mikoa yote.”
Mkutano wa kupunguza umaskini duniani
Hivi karibuni, China ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa ngazi ya juu wa kupunguza umaskini na kupata maendeleo.
Kwa mujibu wa mtandao wa cri.cn, nchi hiyo ilitoa mwito wa kupunguza umaskini na nguvu kubwa ya kuhimiza shughuli za kupunguza umaskini duniani huku ikiwa imepata mafanikio makubwa ya kuigwa na nchi nyingine duniani.
Mtandao huo ulimkariri, naibu waziri mkuu wa China Wang Yang akisema kuondokana na umaskini ni matumaini ya pamoja ya binadamu wote na ni mada muhimu ya dunia ya hivi sasa
“China inapenda kushirikiana na nchi mbalimbali kufanya mawasiliano kuhusu uzoefu wa kupunguza umaskini, kuhimiza ushirikiano wa kimataifa kwenye kupunguza umaskini na kupata maendeleo, na kutilia nguvu kubwa ili kutimiza lengo la ajenda za maendeleo endelevu za mwaka 2030.”
Katika mkutano huo, mafanikio ya China yalisifiwa na pande mbalimbali. Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Jose Graziano da Silca alisema asilimia ya 80 ya watu maskini duniani wako vijijini na uzoefu wa China kwenye kupunguza umaskini katika maeneo hayo ni mfano mzuri.
“China inahimiza maendeleo ya kilimo bila kusita, na kuinua kiwango cha maisha ya watu maskini kwa kiasi kikubwa. Katika miaka 30 iliyopita, China imewasaidia watu milioni 700 kuondokana na umaskini. Sisi tunaisifu China kwa kuweka lengo lake la kupunguza umaskini, ambalo limewekwa kabla ya miaka 10 kuliko lengo la ajenda za maendeleo la mwaka 2030 la Umoja wa Mataifa. Na uzoefu wa China unatakiwa kuigwa na nchi nyingine.”
Katika ufunguzi wa mkutano huo, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye pia ni naibu mkurugenzi wa shirika la mpango wa maendeleo la umoja huo Tegegnework Gettu, alisoma barua ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akisema kupunguza umaskini kwa malengo madhubuti ni njia ya pekee ya kutimiza lengo la ajenda za maendeleo endelevu la mwaka 2030.
Alisema siku zote China inafanya juhudi kukabiliana na changamoto, na kutekeleza mfumo wa kujiendeleza kwa pande zote. Alieleza imani yake kuwa China itaendelea kupunguza idadi ya watu maskini, kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini, kati ya mijini na vijijini, kati ya sehemu za Mashariki za Pwani na sehemu za Bara na kwamba uzoefu wa nchi hiyo unaweza kuigwa na nchi zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment