Rais Faure Gnassingbe amesikitishwa na jinsi mitandao ya kijamii inavyotumika kumchora kama mtu mbaya katika kipindi ambacho maelfu ya wafuasi wa upinzani wakitoa wito ajiuzulu.
Hii ndiyo kauli yake ya kwanza dhidi ya maandamano ya kupinga serikali yake yaliyoanza Agosti wakitaka kurejeshwa kwa Katiba yam waka 1992 iliyotaja vipindi viwili vya miaka mitano mitano ya urais pamoja na mfumo wa raundi mbili za upigaji kura.
“Leo wale wanaolewesha, wanaosema uongo, wamepata washirika wapya teknolojia na wanaweza kukigeuza kitu cha kweli au mtu wa kawaida kama mimi aonekane dikteta mumwagaji damu. Lakini siku chache zijazo, ukweli utashinda,” Gnassingbe aliwaambia maelfu ya wajumbe wa chama tawala cha Union for the Republic (UNIR) mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Nilichaguliwa na siku chache baadaye ukweli utadhihirika. Inahitaji moyo, uvumilivu na ujasiri kuyashinda majaribu na tunaweza,” alisema mbele ya umati huo kwenye mji wa Tsevie, kilomita 35 kaskazini mwa mji mkuu Lome.
Mgogoro wa kisiasa nchini Togo mpaka sasa umesababisha vifo vya watu 16 na wengi wao wamejeruhiwa katika maandamano yanayoandaliwa na muungano wa vyama vya upinzani ambavyo vimeapa kwamba havitarudi nyuma hadi Gnassingbe aachie madarakani.
Baraza la mawaziri liliwasilisha bungeni muswada mapema Septemba yalipopamba moto maandamano ya kushinikiza ukomo wa mihula ya rais urejeshwa kama ilivyopitishwa na Katiba iliyoandaliwa na hayati baba yake Faure Gnassingbe.
Upinzani ulikataa muswada huo uliolenga kurekebisha Ibara ya 59 ya Katiba ambayo imeendelea kukiacha kifungu kinachosema “hakuna mtu wa kutumikia zaidi ya mihula miwili”.
No comments:
Post a Comment