Wednesday, November 1

WATAALAM JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAIBUA CHANGAMOTO SEKTA YA NISHATI


Watalaam wa Masuala ya Nishati wakifuatilia taarifa kuhusu masuala ya umeme wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Asteria Muhozya, Arusha

Wataalam wa Masuala ya Nishati wanaoshiriki Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki unaondelea jijini Arusha wameibua masuala kadhaa katika mkutano huo ambayo yanalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya Nishati iliyokubaliwa na Jumuiya hiyo. Hayo yalibainika katika siku ya Pili ya mkutano wa Timu ya Wataalam kutoka Jumuiya hiyo ulioanza tarehe 30 Oktoba, 2017. Mkutano wa Wataalam umefanyika kabla ya kikao cha Makatibu Wakuu kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, 2017 na kitafuatiwa na kikao cha Mawaziri wa Nishati kinachotarajiwa kuhitimisha mkutano huo tarehe 3 Oktoba,2017.

Baadhi ya miradi ya umeme iliyojadiliwa ni pamoja na ile ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme inayounganisha nchi na nchi ambayo imeelezwa kuwa na kasi ndogo katika utekelezaji wake. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa Miundombinu ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 wa Singida- Arusha- Namanga, mradi wa kV 220 wa Rusumo- Nyakanazi na mradi wa kV 400 wa Iringa- Mbeya - Tunduma. Pia, Wataalam hao wamejadili masuala ya kodi kwa vifaa vya umeme jua, miradi ya umeme ya mipakani ikiwemo miradi ya Murongo/Kigagati na Nsogezi pamoja na Sera ya Usalama wa Nishati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baadhi ya Wataalam kutoka Tanzania wakijadiliana jambo wakati wa mkutano huo.

Aidha, katika siku mbili za majadiliano, Watalaam kutoka Jumuiya hiyo pia wamejadili masuala kadhaa yakiwemo yanayohusu nishati jadidifu, gesi asilia na mafuta. Kikao cha Makatibu Wakuu, kitakachofanyika tarehe 2 Oktoba, kitatanguliwa na kikao cha Kamati ya Nishati cha Baraza hilo kinachofanyika leo tarehe 1 Oktoba, 2017 ambapo hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Wataalam hao zitajadiliwa katika kikao hicho.

Awali, akifungua mkutano wa Baraza hilo kwa upande wa Wataalam tarehe 30 Oktoba, 2017 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Sekta za Kijamii na Uzalishaji, Christophe Bazivamo alieleza umuhimu wa nchi husika kuongeza kasi ya upatikanaji wa Nishati miongoni mwa nchi wananchama ili kuwezesha mapinduzi ya Viwanda na kusisitiza kuwa, miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ya Jumuiya hiyo ni Nishati.
Wataalam kutoka nchi mbalimbali wakijadiliana kuhusu masuala ya mafuta na gesi asilia wakati wa Mkutano wa 12 wa Baraza la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Bazivamo aliongeza kuwa, ili nchi hizo ziendeleee kiviwanda zinahitaji nishati kwa kuwa ndiyo kichocheo kikuu cha maendeleo na kwamba, bado idadi kubwa ya wananchi wa jumuiya hiyo haijaunganishwa na nishati ya umeme. Pia, aliongeza kuwa, ukosefu wa nishati hiyo siyo tu unadidimiza maendeleo ya watu pia unaathiri sekta ya elimu kwa kuwa, kukosekana na nishati kunasababisha wanafunzi hususani waishio vijijini kutumia muda mwingi kutafuta nishati ya kuni kwa ajili ya kupikia badala ya kujikita na masomo.

Nchi zinazoshiriki mkutano huo ni pamoja na Tanzania, Uganda, Rwanda, Uganda na Kenya. Aidha, Tanzania inawakilishwa na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Mazingira na Nishati ya Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Wakala wa Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta , Zanzibar (ZURA). Mwenyekiti wa Mkutano wa 12 wa Baraza hilo ni nchi ya Uganda na Katibu ni nchi ya Rwanda.
Baadhi ya Wataalam kutoka nchini Kenya wakijadiliana jambo.

No comments:

Post a Comment