Katika baraza hilo jipya Rais Magufuli ameonekana kuwateua wabunge wengi ambao wameingia bungeni kwa mara ya kwanza.
Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuingia bungeni kuwatumikia wananchi wa Pangani, Jumaa Awesu ameteuliwa kwenye baraza la mawaziri kutumia nafasi ya naibu waziri wa maji.
Mbunge wa Viti maalum anayewakilisha kundi la walemavu, Stella Ikupa anaweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka kwenye kundi hilo kuingia ndani ya baraza kuitumikia nafasi ya naibu waziri anayeshughulikia masuala ya walemavu.
Mwanasiasa machachari na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola naye amechomoza kwenye baraza hilo kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Mbunge wa Maswa Mashariki, Haroon Nyongo anaingia kwenye baraza la mawaziri kusaidiana na Angela Kairuki kuiongoza wizara ya madini.
Ukiacha huyo pia Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga ameingia kwenye baraza hilo kutumikia nafasi ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Pia Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu naye ameingia kwenye baraza hilo kutumikia Wizara ya Nishati kama naibu waziri.
Wizara hii inatajwa kuwa na changamoto lukuki ikiwemo kukosekana kwa umeme wa uhakika hasa katika kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya tano inalenga kuifanya Tanzania nchi ya viwanda.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa naye kwa mara ya kwanza ameingia kwenye baraza la mawaziri kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Bahati imeendelea kuwa njema kwa Mkoa wa Pwani kwani Mbunge wa Mkuranga, Abdala Ulega ameingia kwenye baraza hilo kutumika kama naibu waziri katika wizara mpya ya mifugo na uvuvi.
Juliana Shonza aliyejipatia umaarufu baada ya kunusurika kupigwa na wabunge wa Chadema, naye ameingia kwenye baraza hilo kama Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mbunge wa Muhambwe, Atashasta Nditiye anaingia kwenye baraza hilo kama Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi akishughulikia masuala ya Ujenzi na Uchukuzi.
Elias Kwandikwa ameingia kwenye wizara hiyo kama naibu waziri anayeshughulikia masuala ya mawasiliano.
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile anaingia kwenye baraza jipya kama Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Josephat Kandege na Joseph George Kakunda wameingia kwenye baraza hilo kama manaibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
No comments:
Post a Comment