Dar es Salaam. Mwadhama Kadinali, Polycarp Pengo amesema kwamba kauli iliyotolewa hivi karibuni naAskofu wa Jimbo la Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi kwamba Katiba mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi ni maoni binafsi siyo msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.
Pengo alisisitiza hilo wakati akitoa ufafanuzi juu ya sintofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa kanisa hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.
“Napenda kutamka moja kwa moja kwamba huo siyo msimamo wa kanisa na hauwezi kuwa msimao wa kanisa kwa sababu sisi tuna taratibu zetu za kuishauri Serikali au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.
Alifafanua zaidi kwamba kutokana na nafasi ya Uaskofu aliyonayo Askofu Niwemugizi, kauli yake inaweza kutafsiriwa kuwa ndio msimamo wa Kanisa Katoliki au wa Jimbo la Rulenge, Ngara lakini kimsingi kauli ile imekosa vigezo vya kuichukulia kama msimamo wa kanisa au jimbo anakotoka.
Kadinali Pengo alisema yeye binafsi kipaumbele chake ni kuona huduma za jamii kama zile elimu na afya zinaendelea kuboreshwa kwa kasi kama ambavyo Serikali ilivyoanza kufanya.
“Mtu akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba mpya. Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka.
“Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kadinali Pengo.
Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Marek Solczynski hakutofautiana na kauli ya Kadinali Pengo kwa kusema pamoja na kwamba Askofu Niwemugizi ana haki ya kutoa maoni yake lakini tatizo linakuja pale watu wakaposhindwa kung’amua kuwa ni maoni binafsi au ni ya kanisa.
Amesisitiza kwamba kanisa lina taratibu zake za kutoa maoni kwa masuala ya kijamii na kwa Serikali. “Hayo ni maoni yake binafsi na wala yasihusishwe na kanisa katoliki,” alisema Balozi Askofu Merek.
Hivi karibuni Askofu Niwemugizi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kipaumbeke cha kwanza cha Watanzania ni Katiba mpya na kuongeza yeye binafsi ni miongini mwa watu walioipinga Katiba Inayopendekezwa.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo walisema, pamoja na mjadala mkubwa ulioibuka na baadhi ya wanasiasa kususia mchakato wa kukamilisha Katiba mpya, wataalamu wa sheria wanasema Katiba inayopendekezwa ilikuwa ni bora kuliko ya sasa ikiwemo kuruhusu wagombea kuhoji mahakamani matokeo mbalimbali ikiwemo ya urais.
“Hata mimi ukiniuliza leo tuache kufanya mageuzi ya msingi katika jamii ili kuwa na uchumi imara au tuanze kushughulika na Katiba mpya, nitakwambia tuachane na Katiba.
“Nakumbuka ile Katiba Inayopendekezwa ilikuwa na masuala makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo kipengele cha kupinga matokeo ya urais lakini kwa kuwa kuna watu walikuwa na maslahi yao binafsi, wakatoka nje ya Bunge na kukwamisha mchakato ule sioni uharaka wa leo tuache mengine yote turejee kwenye mchakato huu,” alisema Wakili wa Mahakama Kuu, James Nandonde.
No comments:
Post a Comment