Saturday, October 7

Walaani unyama Cameroon, wakemea mapepo Uganda


Yaounde, Cameroon. Watumishi wa Mungu, baada ya kuona yanayoendelea Cameroon na Uganda, wamejitokeza na kupaza sauti zao kukemea pepo anayeelekea kuchafua hali ya hewa ya siasa na amani.
Kutoka Yaounde, maaskofu wa Kikatoliki wamelaani “unyama” na “matumizi yasiyo ya lazima” ya nguvu dhidi ya waandamanaji katika eneo la wanaozungumza Kiingereza wiki iliyopita yaliyosababisha kuuawa watu 19.
Mapambano hayo yalitokea wakati viongozi wa eneo hilo walipoashiria kujitangazia uhuru wakidai kwamba Wanaozungumza Kiingereza kwa miongo mingi wamekuwa wakikosa usawa kiuchumi na kukosa haki za kijamii mbele ya wenzao walio wengi wanaozungumza Kifaransa.
"Tunalaani kwa nguvu zetu zote unyama na matumizi ya silaha za moto yasiyo ya lazima dhidi ya raia ambao wala hawakuwa na silaha yaliyofanywa na vikosi vya sheria na usalama hata kama walichokozwa,” ilisema taarifa ya Baraza la Maaskofu jimbo la Bamenda.
Watu 14 waliuawa katika mapambano na vikosi vya usalama wiki iliyopita, na wafungwa watano walipigwa risasi na walinzi walipojaribu kuvunja gereza la Kumbo.
Baadhi ya waombaji walipigwa mabomu ya kutoa machozi walipokuwa wakiondoka katika misa wakati wengine “walikamatwa, kujeruhiwa na baadhi (wakiwemo vijana wasio na silaha na wazee) walipigwa risasi kutoka kwenye helikopta.”
Lakini serikali imejitetea kwa kusema askari wake walilazimika kujihami baada ya kuweka amri ya kutotemba katika eneo hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na shirika la kutetea haki za binadamu la and Amnesty International wametoa wito ufanyike uchunguzi.
Kutoka Kampala Uganda, waumini wapatao 100 wakiongozwa na mchungaji Julius Oyet, walikwenda bungeni ambako walifanya ibada, wakalitakasa Bunge kwa damu ya Jesu kisha wakamwekea mikono kichwani Spika wa Bunge Rebecca Kadaga.
Watumishi hao wa Mungu waliombea utakaso ili Bunge lirejea katika hali yake ya kawaida baada ya wiki iliyopita kukumbwa na vurugu zilizosababisha wabunge kadhaa kujeruhiwa na wengine wa upinzani kukamatwa na polisi.
Wabunge 24 wa upinzani walisimamishwa Septemba 27 baada ya vurugu kuibuka huku wakimtuhumu Waziri wa Maji Ronald Kibuule kuingia na bunduki. Mgawanyiko mkubwa ulijitokeza wakati wa mjadala wa ukomo wa umri wa rais.
“Tunaomba hekima na mwongozo wenye mwelekeo. Tunatangaza kwamba hakuna silaha itakayofanya kazi dhidi yake na wala hatakufa mapema,” alisema Oyet akiwa amemwekea mikono Spika.
Katika sala zake, Mchungaji Tony Okot kutoka Kaskazini mwa Uganda alisema: “Tunaombea amani katika bunge hili na mzunguko wa viongozi wakati tukiomba utulivu wa wabunge wanapojadili muswada na kunyamazisha mapepo mengine yasifike hapa. Tunaomba kuwa chochote wanachofanya wafanye kwa hofu, amani, upendo, umoja na kuheshimiana.”

No comments:

Post a Comment