Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo akiongoza askari kuhamisha udongo "Kifusi" toka kwenye msingi wa ujenzi wa nyumba za Polisi na kupeleka kwenye mtaro.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Ujenzi wa kituo kidogo cha Polisi cha Morombo kilichopo kata ya Murieti halmashauri ya Jiji la Arusha huenda ukawa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo ambalo linakuwa kwa kasi kibiashara na ongezeko la idadi ya watu.
Uwepo wa kituo hicho utawezesha kusogeza huduma ya kiusalama kwa wakazi hao kwa ukaribu zaidi lakini pia kesi zao zitaripotiwa hapo hapo badala ya Kituo kidogo cha Sombetini au kituo Kikuu ambavyo vipo umbali mrefu toka eneo hilo.
Akizungumza katika eneo la kituo hicho, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba ufunguzi wa kituo hicho ambacho kipo kwenye hatua za umaliziaji unatarajia kwenda sambamba na wa nyumba za askari watakaofanya kazi kituoni hapo na hiyo itasaidia askari kutoa huduma kwa haraka na ukaribu kwa kuwa watakuwa wanaishi eneo hilo.
Kamanda Mkumbo alisema kwamba, yeye pamoja na askari wapatao 200 wa vikosi mbalimbali jana waliamua kushiriki katika kuchimba msingi na kubeba udongo “Vifusi” kutoka eneo la ujenzi na kwenda kuumwaga kwenye mtaro.
Alisema pamoja na majukumu walionayo ya kuhakikisha jiji la Arusha pamoja na wilaya nyingine za mkoa huu zinakuwa salama lakini pia wameamua kufanya hivyo kwa nia ya kupunguza gharama na watakuwa tayari kushiriki katika kusogeza matofali kwa mafundi na hata kukoroga zege pindi nguvu kazi itakapohitajika.
“Pamoja na sisi kujitoa kufanya kazi hizi lakini pia wananchi wanaozunguka eneo hilo wanapaswa kujitolea kubeba vifusi kwa kuwa kituo hicho ni cha kwao”. Alitoa wito huo Kamanda Mkumbo.
Kwa upande wake mkazi wa eneo hilo aliyejulikana kwa jina la mzee Isihaka Kivuyo alisema kwamba, kituo hicho kitasaidia kuiweka jamii karibu na jeshi hilo jambo ambalo litasaidia kupunguza uhalifu.
Alisema kwamba wananchi wanatakiwa wafurahie ujenzi wa kituo hicho hivyo na kuwataka wajitolee katika shughuli ndogondogo za ujenzi wa nyumba hizo za askari badala ya kazi hizo kufanywa na askari Polisi pekee ambao wana majukumu mengine ikiwemo kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unakuwepo.
Ujenzi wa kituo hicho chenye hadhi ya daraja B ambao umefadhiliwa na Kampuni ya Lodhia Group ulianza toka mwaka 2016 mwezi Mei, lakini pia ujenzi wa nyumba saba za askari kwa sasa upo kwenye hatua za uchimbaji wa msingi na unatarajiwa kwenda kwa kasi ili uende sambamba na ufunguzi wa kituo.
Baadhi ya askari wakichimba na kubeba udongo toka eneo la ujenzi wa nyumba saba za askari kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya ujenzi.
Kituo kipya cha Polisi Mrombo kilichopo kata ya Murieti halmashauri ya jiji la Arusha ambacho kina hadhi ya daraja "B" kipo katika hatua za mwisho za umaliziaji.
No comments:
Post a Comment