Saturday, October 14

TUMUENZI BABA WA TAIFA KWA KUIGA MAISHA YAKE-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba Watanzania waendelee kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kwa kuiga maisha yake na utendaji wake.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 14, 2017) aliposhiriki ibada maalumu ya kumuombea Mwl. Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar.

Ibada hiyo ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Mwl. Nyerere ni sehemu ya maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru uliozimwa leo katika mkoa wa Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.

Katika Idaba hiyo Waziri Mkuu amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanamuenzi Mwl. Nyerere kwa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.Awali, Katibu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Padri Cosmas Shayo ambaye aliongoza ibada hiyo aliwaomba waamini wamuenzi Mwl. Nyerere kwa kudumisha umoja na mshikamano wa Taifa.

“Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere aliwapenda watu wote bila kujali Imani zao wala itikadi zao. Alikuwa mzalendo na alitaka Watanzania waishi maisha bora.”

Padri Shayo aliongeza kuwa tunu za amani na umoja zilikuwa miongoni mwa falsafa kuu ya Mwl. Nyerere, ambapo matokeo yake ni umoja na mshikamano wa Taifa uliopo.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Balozi Seif Ally Idd, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Bi Jenista Mhagama, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa.

Wengine ni Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Bi. Mauldine Castico, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira Bw. Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Walemavu Bi. Stella Alex Ikupa na mwakilishi wa familia ya Mwl. Bw. Makongoro Nyerere.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMAMOSI, OKTOBA 14, 2017.         

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa kwenye ibada maalum ya kumuombea Mwalimu Julius Nyerere, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar (katikati) ni Makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) ni Mke wa Waziri Mkuu mama Marry Majaliwa. Oktoba 14, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waumini waliyo hudhuria kwenye ibada maalum ya kumuombea Mwalimu Julius Nyerere, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar, Oktoba 14, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)    

No comments:

Post a Comment