Friday, November 24

Kenyatta amwalika Odinga


Nairobi, Kenya. Rais Uhuru Kenyatta amemwalika “kaka” yake na mshindani wake mkuu Raila Odinga kuhudhuria katika sherehe za kuapishwa kwake Jumanne ya Novemba 28 zilizopangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Kasarani.
Wengine walioalikwa ni wagombea sita wa urais walioshindana na Rais Kenyatta kwanza katika uchaguzi uliobatilishwa na Mahakama ya Juu na pili wa marudio uliofanyika Oktoba 26.
“Wagombea wengine saba wa urais na wagombea wenza wao katika uchaguzi wa mwisho wa urais wamepewa mwaliko kuhudhuria sherehe hizo,” mwenyekiti wa timu ya watu 22 ya maandalizi ya sherehe, Joseph Kinyua amewaambia waandishi wa habari Ijumaa.
Wagombea wengine na wagombea wenzao wao kwenye mabano ni Joseph Nyagah (Moses Marango); Abduba Dida (Titus Ngetuny);  Ekuru Aukot (Emmanuel Nzai) na Japheth Kaluyu ( Muthiora Kariara).
Katika orodha ya wageni waalikwa wamo Cyrus Jirongo (Joseph Momanyi); Michael Wainaina (Miriam Mutua) na Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka.
“Kwa kuwa tukio hili la kitaifa lina umuhimu mkubwa, serikali ya Kenya katika ngazi zote mbili na matawi yake matatu itawakilishwa kikamilifu,” alisema.
Odinga alijiondoa kwenye uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 akilalamikia kutofanyika marekebisho muhimu katika tume ya uchaguzi na akatoa wito ufanyike uchaguzi mkuu katika muda wa siku 90 chini ya tume mpya ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment