Friday, November 24

Dk Shika ataka asifuatiliwe kutimiza ahadi


Kahama. Dk Louis Shika, ‘bilionea’ aliyejizolea umaarufu baada ya kuibuka mshindi katika mnada wa nyumba za mfanyabiashara maarufu, Said Lugumi, bado anaendeleza vituko; safari hii amesema hataki kufuatiliwa.
Dk Shika alijizolea umaarufu baada ya kuibuka kwenye mnada huo na kutaja viwango vya juu vya fedha kuwapiku watu wengine waliojaribu kununua nyumba hizo.
Lakini akashangaza baada ya kushindwa kulipia hata asilimia 25 ya takriban Sh3 bilioni ya nyumba tatu alizoshinda mnada licha ya kuahidi kuwa angefanya hivyo ndani ya muda mfupi kwa sababu fedha zake ziko nchini Urusi.
Kauli zake katika mnada huo, hasa ya "900 itapendeza", ndizo zilizompa umaarufu kiasi cha kupata udhamini wa kampuni tofauti, lakini bado hajaisha vituko.
Akiwa mjini Kahama mkoani Shinyanga jana Alhamisi (Novemba 23,2017) kuhudhuria mahafali ya Chuo cha Afya, msomi huyo wa Urusi aliahidi kukifadhili chuo hicho Sh2.2 bilioni kila mwaka.
Hata hivyo, mtaalamu huyo wa utabibu wa binadamu ameutahadharisha uongozi wa chuo hicho, akiutaka kutomfuatilia kudai kutimiza ahadi yake kwa kuwa anataka kuepuke mambo ya mnada wa nyumba kujirudia.
“Inapendeza tu mkiamini kwamba mtakuwa mnapokea kiasi hicho cha fedha (dola milioni moja), kila mwaka,” alisema Dk Shika.
Dk Shika pia aliwatahadharisha waandishi wa habari kutomuuliza kuhusu kutimiza ahadi hiyo ya dola milioni moja kwa chuo ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa kwa sababu hana fedha taslimu hadi mchakato aliosema wa kuhamisha fedha kutoka Urusi utakapokamilika.
Akizungumza na jumuiya ya chuo na wageni waalikwa, Dk Shika ametaja sababu ya kuahidi msaada huo kuwa ni kukiwezesha kutoa elimu bora ya utabibu na masuala ya afya ambayo ni muhimu kwa jamii na maendeleo ya Taifa.
Dk Shika aliwasili Kahama kwa ndege iliyotua uwanja wa ndege wa Buzwagi na kupokewa na mkuu wa chuo hicho, Yona Bakungile, huku msafara wake ukiwa na magari zaidi ya 50 yaliyopita mitaa mbalimbali kabla ya kufika chuoni.
Chuo hicho kipo Kata ya Mwendakulima umbali wa takriban kilomita tatu kutoka mji wa Kahama.
Dk Shika, mbele ya mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhil Nkurlu aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya kwanza, alitoa ahadi hiyo baada ya Bakungile kuzungumzia changamoto ya baadhi ya wanafunzi kukatisha masomo kutokana na wazazi na walezi kushindwa kuwalipia ada.
“Baadhi ya wanafunzi pia wamekatisha masomo kwa kukosa ada baada ya wazazi au walezi wao kufariki dunia,” alisema Bakungile.
Akizungumzia ahadi ya Sh2.2 bilioni kwa chuo chake kila mwaka, Bakungile alisema anaamini na "itapendeza akizipokea" kwa sababu zitasaidia kuinua kiwango cha taaluma na ubora wa miundombinu chuoni.

No comments:

Post a Comment