Friday, November 24

Nyota wa Real Madrid wapewa bure magari ya kifahari


Nyota wa klabu ya Real Madrid jana Alhamisi walisherehekea siku ya udhamini wa kampuni ya Audi kwa kushindana katika mbio zisizo halisi za magari aina ya Formula E kabla ya kila mmoja kukabidhiwa gari la kifahari aina ya Audi.
Hafla kwa timu hiyo ambayo ni maarufu kwa jina la Los Blancos, ilifanyika kwenye uwanja wa mpira wa kikapu uliopo Real Madrid City na iliandaliwa na kampuni ya kutengeneza magari ya Ujerumani ya Audi kusherehekea udhamini kwa mabingwa hao wa soka wa Hispania, kwa mujibu wa gazeti la Mirror la Uingereza.
Wakiwa wamevalia suti za michezo, vijana wa Zinedine Zidane walionyeshana ukali wao katika kuendesha magari katika mashindano yasiyo halisi katika kutaka kujua mbabe miongoni mwao.
Dani Carvajal aliibuka kuwa mshindi, akimuacha Sergio Ramos, ambaye alishika nafasi ya pili, na Marco Asensio aliyekuwa wa tatu.
Baada ya mbio hizo, Audi ilimzawadia kila mchezaji gari mpya kabisa, zawadi ambayo kila mchezaji hupewa kila mwaka.
"Audi imekabidhi magari rasmi kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Real Madrid kwenye Uwanja wa Mpira wa Kikapu uliopoReal Madrid City," imeandika tovuti ya klabu hiyo.
"Florentino Pérez na Guillermo Fadda, mkurugenzi wa Audi nchini Hispania, walihudhuria hafla hiyo. Wakiwa wamevalia suti za michezo, wachezaji walifurahia mbio za magari ziszo halisi za Formula E ambazo ziliandaliwa na kampuni hiyo ya magari ya Ujerumani."
Tovuti hiyo inasema baada ya kupiga picha ya pamoja ya washindi na ile ya kila mwaka ya wachezaji wote, viongozi wa Real Madrid na Audi walipeana zawadi.
"Florentino Pérez alimpa Francisco Pérez Botello, rais wa Volkswagen Hispania, na Guillermo Fadda mashati maalum kwa ajili yao, na akapokea usukani kutoka Audi ABT Formula E," inasema tovuti ya Real Madrid.
"Baadaye wacheaji wa kikosi cha kwanza na Zinedine Zidane walikabidhiwa magari mapya kila mmoja kwa ajili ya msimu wa mwaka 2017-2018."

No comments:

Post a Comment