Mtanzania mwenye kuipenda nchi yake, jambo la kwanza ataomba utaifa uheshimiwe. Utaifa una pande mbili; mosi ni amani, utulivu na mshikamano. Pili ni ustawi wa hali za kimaisha. Katika kushughulikia yote hayo lazima kuwe na usawa. Hivyo basi, ulinzi namba moja wa utaifa ni kuwapo kwa usawa miongoni mwa wananchi.
Usawa haupatikani kwa kadirio lenye kugawiwa na mtu mmoja au kikundi cha watu. Usawa huratibiwa kwa mujibu wa Katiba. Maana Katiba ndiyo mfumo na utaratibu wa kimaisha ambao wananchi wanakuwa wamekubaliana kuufuata. Hivyo basi, kuendesha nchi kwa ridhaa ya makundi yote ni lazima Katiba ifuatwe.
Kuvunja Katiba kuna tafsiri mbili; ya kwanza ni kuharibu utaratibu wa kimaisha ambao nchi iliazimia kuuishi. Pili ni kuwagawa watu. Kwa maana hiyo, jaribio lolote la kuvunja Katiba linabeba sura ya kuharibu utaifa. Kwani utaifa hauwezi kuonekana kwenye jamii iliyogawanywa, ama kikabila au kidini, hata kwa matabaka ya kiuchumi na itikadi za kisiasa.
Tanzania siyo nchi ya chama kimoja cha siasa. Kila chama kilichosajiliwa kisheria kina haki ya kuendesha shughuli zake za kisiasa ilimradi kisivunje Katiba na sheria za nchi. Kuzuia vyama kufanya shughuli zao halali za kisiasa ni kuvunja Katiba. Chama kimoja kupata upendeleo kuliko vingine ni kuwagawa wananchi. Usawa ndiyo ngao ya utaifa.
Kila Mtanzania anao uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa au kuishi bila chama. Uhuru huo siyo zawadi bali ni haki yake ya kikatiba. Na kwa utashi wake huo, anayo haki ya kuhudumiwa na Serikali Kuu, vilevile Serikali za Mitaa bila kubaguliwa. Kwa kuzungumzia eneo hili, hatuwagusi wafanyakazi wa umma ambao masharti yao ya ajira yanawabana kujihusisha na vyama vya siasa.
Tanzania ni ya maskini na matajiri. Asiwepo kiongozi wa kujenga huruma na maskini au awe upande wa matajiri na kuwakandamiza maskini. Ubaguzi wa matabaka ya kiuchumi ni hatari mno. Wachina walipogawanywa kwa matabaka, ilitokea vita kati ya chama cha mabwanyenye, Kuomintang, dhidi ya Communist cha makabwela. Mpaka mwaka 1949, jumla ya watu milioni nane walikuwa wamepoteza maisha na wengine kupoteza viungo.
Tafakuri ya maaskofu
Februari mwaka huu, wakati wa kuelekea kuanza kwa kipindi cha siku 40 za toba ya Kwaresma, Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), lilitoa waraka kuhusu hali ya kisiasa na kijamii ilivyo nchini na kugusia, vilevile kuonya yale mambo ambayo viongozi hao wa Kanisa Katoliki waliona yanahitaji masahihisho au utatuzi.
Machi 15, mwaka huu, maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), walikutana na kuandika waraka kwa waumini wao na Watanzania kwa jumla. Waraka huo waliuita Ujumbe wa Pasaka wa Baraza la Maaskofu wa KKKT. Kilichomo humo ni maonyo juu ya mambo ambayo viongozi hao wa kiroho wameona hayapo sawa.
Ukipitia hoja zote, kile ambacho kimezungumzwa na maaskofu wa Kanisa Katoliki na KKKT kinalenga kujenga utaifa. Unaweza kuiona shabaha ya viongozi hao kwamba wanalilia usawa. Anayehubiri usawa ndiye mwenye kustawisha upendo. Hakuna jamii inayoweza kupendana ikiwa watu wake hawaoni usawa miongoni mwao. Jamii iliyogawanywa kamwe haitapendana.
Maaskofu wanataka Katiba iheshimiwe, maana hiyo ndiyo ilani kuu ya maisha ya watu kwenye nchi yao. Yeyote mwenye kutetea Katiba ndiye mlinzi wa utaifa. Anayetetea au kulinda utaifa huyo anataka usawa, kwa hiyo ndiye mwenye kuipiga jamii yenye upendo. Sasa basi, unawezaje kuwapinga maaskofu? Ni rahisi kumtafsiri kila anayewapinga maaskofu kuwa haipendi Tanzania. Mpingaji huyo akiwa Mtanzania, maana yake si Mtanzania mzuri.
Haivutii kuona watu wanapaza sauti kuwasema maaskofu, wengine wanawashambulia binafsi. Unaweza kujiuliza; kweli maaskofu wamefanya makosa kutoa waraka wenye kuagiza Katiba iheshimiwe? Maaskofu wanatenda kosa kusema kwamba usawa na haki katika ufanyaji wa shughuli za kisiasa vinapokosewa kutasababisha machafuko? Yaani maaskofu waone mambo hayapo sawa kisha wao wanyamaze tu!
Viongozi wa dini wanapaswa kuhubiri upendo, maana maandiko matakatifu yanasema jamii yenye watu wasiopendana haiwezi kuuona ufalme wa Mungu. Popote panapokosekana upendo basi na chuki huchipua. Maaskofu wanaona jinsi ambavyo chuki inainyemelea nchi. Watu wanataka maaskofu wakae kimya, wasiikemee chuki. Kuwapinga maaskofu kunahitaji moyo wa kikatili dhidi ya Tanzania.
Waraka wa TEC
Waraka wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC) ulisainiwa na maaskofu 36. Ulielezea mazingira ya utawala bora kuwa ni mabaya Tanzania. Uligusia jinsi ambavyo shughuli za kisiasa zinavyopigwa marufuku, wakati ni shughuli halali kikatiba na kwa sheria za nchi. Maaskofu hao walieleza kwamba makongamano, maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama haipaswi kuzuiwa.
Kabla ya kuelezea hali ya kisiasa nchini ambayo kwa tafsiri ya maaskofu ni mbaya, walitoa neno lenye kuuliza, je, kila mmoja ni mlinzi wa mwenzake? Neno ambalo asili yake ni Biblia, pale Cain ambaye ni mtoto wa Adam, alipoulizwa kwa sauti ya Mungu alipo mdogo wake Abel. Cain alijibu: “Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
Hivyo, TEC katika waraka wao walisisitiza kuwa na dhamira njema kwa kila mtu kujiona ni mlinzi wa mwenzake. Jamii isome alama za nyakati ili kuwezesha maisha bora yenye maelewano. Yote ambayo yamesemwa na TEC, uponyaji wake upo kwenye dhamira njema. Katiba ya nchi iheshimiwe. Shughuli halali zisiharamishwe kwa sababu ya matakwa binafsi. Kama walivyosema maaskofu, haya mambo ya watu kuona wananyimwa haki zao, husababisha matokeo mabaya, hasa wahusika wanapoona ni lazima wazipate na kuanza kuzidai kwa njia zenye shari.
TEC walisema kuhusu kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na baadhi ya vyombo kufungiwa, kwamba kunapunguza haki ya kimsingi ya Watanzania kupata habari katika wigo mpana. Walisema pia kwamba Mahakama na Bunge ambayo ni mihimili huru ya dola, inayopaswa kujisimamia kutekeleza majukumu yake ya kikatiba, haipo huru kwa sasa.
Kimsingi waraka wa TEC uligusa maeneo mengi, lakini yaliyohusu siasa ni hayo. Ukishayapitia jiulize; kuna ubaya gani wamefanya? Ni kweli kwamba shughuli za siasa zimepigwa marufuku. Kuna wabunge wananyimwa mpaka fursa ya kukutana na wapiga kura wao ili kujadili maendeleo na uwakilishi wao kwa jumla.
Hayo yapo wazi na inafahamika kuzuia hayo ni kinyume na Katiba, vilevile sheria za nchi. Je, maaskofu wakae kimya?
Waraka wa KKKT
Waraka wa maaskofu wa KKKT, ukiwa na kichwa Ujumbe wa Pasaka, katika tafakuri ya nchi, vilevile waraka huo umepewa utambulisho wa “Taifa Letu Amani Yetu” na umesainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo.
Yaliyoguswa ni masuala yenye kuhusu hali za kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mengine muhimu, vilevile waligusia kuhusu kupatikana kwa Katiba Mpya.
Kwa uungwana kabisa, yapo maeneo maaskofu wa KKKT wameipongeza Serikali. Walisema zipo jitihada zinazofanywa na Serikali kuboresha maisha ya wananchi. Maaskofu hao wamekiri kwamba wameshuhudia nia njema kuhusu uvunaji na umiliki wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa zima. Vilevile waliipa heko Serikali kwa jitihada zake za kukusanya kodi ili kujijengea uwezo wa kuihudumia nchi.
Hata hivyo, maaskofu wa KKKT waliitaka Serikali kutambua kwamba sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa maendeleo na si washindani wa Serikali katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Kimsingi maaskofu wana hoja za msingi. Hata mashehe nao wanapaswa kusema wanayoona hayaendi sawa.
Shehe Mussa Kundecha alisema pia jinsi shughuli za kisiasa zinavyoonekana sasa kuwa kama kuna kutoridhika kuhusu uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kuutetea utaifa siyo kuchanganya dini na siasa, bali ni kupigania usawa. Anayewapinga wanaotetea utaifa huyo haitakii mema Tanzania.
Wakataka jitihada za makusudi na za mara kwa mara zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya Serikali na wadau hao ili kuimarisha uhusiano mwema kati ya Serikali na sekta binafsi.
No comments:
Post a Comment