Saturday, March 31

Serikali iingilie kati kero ya mabasi haya


Ndivyo wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaama tulivyoaminishwa awali kwamba Usafiri wa Mabasi ya Mwendo wa Haraka (Udart) baada ya kuanza ungeondoa adha ya foleni, hivyo kutuwezesha kuwahi kwenye shughuli za maendeleo na nyinginezo za kijamii. Lakini hali imekuwa ni tofauti kwani changamoto nyingi zimeibuka na zinatia doa hata nia ya Serikali ya kutaka kuona wakazi wa jiji hili wanapata usafiri wa uhakika ambao ungeondoa kero hasa ya kutumia muda mwingi kwenye foleni. Nasema hivyo kwa sababu tayari kuna tatizo la abiria kukaa vituoni kwa muda mrefu kutokana na mabasi hayo kuchelewa kufika.
Imekuwa si ajabu kwa msafiri kukaa zaidi ya saa moja kituoni asione basi hata moja likipita.
Kwa sababu kuchelewa kwa mabasi kufika kituoni husababisha msongamano wa watu hali inayohatarisha hata afya zao.
Awali, wasimamizi wa mradi huu waliuaminisha umma kuwa kutokana na kasi ya mabasi hayo, abiria sasa angesubiri kituoni kwa angalau dakika tano, kisha kuanza safari.
Ukiacha hilo tatizo la kuchelewa kwa mabasi, lakini pia kwa sasa hakuna mawasiliano kati ya abiria na wahusika kwenye vituo kama ilivyokuwa awali.
Kulikuwa na matangazo ya mara kwa mara yaliyokuwa yakitolewa pindi tatizo lolote likitokea hata kama ni la kuchelewa kwa mabasi kufika katika kituo husika kwa muda uliopangwa, lakini sasa hivi matangazo hayo hayapo tena.
Lakini naamini kwamba hadi sasa Rais atakuwa amesikia malalamiko au kujionea kupitia vyombo vya habari kuhusu kero wanazopata abiria, hali ambayo imewakatisha tamaa wengine ya kutumia usafiri huo, huku baadhi wakiendelea kuutumia kwa sababu hawana njia nyingine ya kusafiri hasa wakazi wengi wa Mbezi Mwisho.
Kwa hiyo inawezekana kabisa kama usafiri huu ungekuwa wa uhakika watu wengi hata wale wanaotumia usafiri wa magari yao binafsi wangevutiwa kuutumia, hii ingekuwa ni sehemu ya kuingiza faida kwa mradi huo.
Udart kama wakiondoa kero hizo, wanamudu kusafirisha abiria wengi zaidi na mapato yao yanaweza kuongezeka mara dufu ya sasa, lakini kwa sasa wanapata abiria kwa sababu daladala za safari za Muhimbili, Kariakoo na Posta zilizuiwa.
Naamini hata kama hatutangaziwi lakini ni wazi kuna hasara hadi sasa ambayo inaweza kuwa imesabababishwa na uongozi au miundombinu, kwani tumeshuhudia katika msimu wa mvua karakana ikiwa imezungukwa na maji na mabasi kushindwa kutoka.
Ingawa inawezekana pia kuna hasara ambayo pengine haihusiani na Udart, lakini ni hasara kwa Serikali pia kwa sababu watu wakikosa usafiri inamaanisha wanashindwa kuwahi kwenye shughuli zao za maendeleo.
Serikali iingilie kati kuhakikisha mradi huu unatoa huduma bora iliyokusudiwa badala ya kuwa kero na kuwakosesha abiria amani kutokana na usumbufu na kukosa uhakika wa safari hasa wakati wa msimu wa mvua.
Tatizo la kujaa kwa maji eneo la Jangwani, Serikali pia iangalie jinsi ya kulitafutia ufumbuzi haraka, ikiwamo kuwatumia wahandisi washauri ambao watasaidia kuhakikisha ufumbuzi wa tatizo la eneo hilo linapatikana.
Nasema hivyo kwa sababu haya ninayojiuliza mimi, ndiyo wanayojiuliza wananchi huko nje, ni kwanini karakana ya mabasi hayo ilijengwa kwenye eneo lile ambalo ni la mkondo mkubwa wa maji yaendayo baharini?
Je! Wahandisi walioshauri kujengwa kwa karakana ile walikuwa na lengo gani?
Pamoja na yote hayo naona siyo wakati tena wa kuendelea kujiuliza maswali hayo tunachotamani wengi hivi sasa ni kupata huduma nzuri, kwamba Serikali ione umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo

No comments:

Post a Comment