Akiwa na Diamond ameshiriki katika mikataba ya matangazo ya Vodacom, Msasani Shopping Mall na Danube.
Hii ndio inapaswa kuwa faida ya umaarufu. Wanamuziki, wanamichezo, waigizaji na wanaopata umaarufu kutokana na namna mbalimbali kwa kiasi kikubwa wanategemea mikataba ya kutangaza bidhaa ili kujiongezea kipato.
Mikataba hii ina fedha nyingi kama msanii atajipanga. Diamond Platnumz ni mmoja kati ya wasanii ghali Afrika Mashariki na Kati. Kampuni ikitaka kufanya kazi naye lazima ijipange. Ameshawahi kuvuta mkwanja mrefu kutoka Coca Cola, Vodacom na Red Gold kwa kupewa ubalozi.
Lakini kupata mkataba wa ubalozi sio kitu rahisi. Kampuni zinajiuliza mara mbilimbili iwapo msanii husika ana thamani inayoendana nayo.
Chris Brown, Oscar Pistorius, Tiger Woods, Cate Moss na wengine waliziingiza katika mgogoro kampuni zilizowapa migogoro baada ya kufanya yanayoenda kinyume na sura ya kampuni.
Hakuna mfanyabiashara anayetaka kujihusisha kwa namna yoyote na mbakaji, ‘mla unga’, mzinzi, mchepukaji, mwizi au mwenye sifa mbaya yoyote.
Wakati mwingine huingia kichwa kichwa bila kufanya utafiti wa kina, lakini utandawazi umerahisisha kazi hiyo, katika viganja vyake anaweza kuzivuta taarifa za msanii.
Kuna msanii wenye sifa hizo?
Watu maarufu hawaishiwi skendo, ziwe za kutengeneza au za kweli. Yapo makosa wanayofanya bila kujua na wanayoyajua.
Kwa kifupi hakuna msanii ‘msafi’ lakini kila mmoja anaweza kujiepusha au kujisafisha.
Ingawa si mfano sahihi kuutumia, lakini kutokana na umaarufu wake inabidi kukumbushia sakata la mwanamasumbwi Manny Pacquiao na kampuni ya Nike ambayo ililazimika kumwamwaga baada ya kutoa kauli zinazokwenda kinyume na mtazamo wa kampuni hiyo.
Pacquiao aliomba radhi hata baada ya kampuni hiyo kusitisha mkataba naye. Miaka miwili baadaye alipewa mkataba mwingine na kampuni hiyo na hapa tunajifunza kwamba kumbe hata kujutia ni dawa.
Kwa mfano unakuta picha chafu za msanii zinavuja mtandaoni au anafanya tukio lolote la aibu, lakini haombi msamaha hata kwa kuonyesha tu kuwa amefedheheka.
Kwa nini Zari anapata mikataba?
Utauliza mbona Zari ana picha chafu mtandaoni. Ni kweli ana video chafu katika mtandao lakini je, alipiga mwenyewe? Je, sio kwamba aliyeipiga alikuwa na lengo la kujipatia fedha kupitia jina la mwanamke huyo? Anajutia? Ndio.
Inapotokea amepiga picha katika vazi la kuogelea au namna yoyote ile lakini ametumia mpiga picha maalumu (proffesional camera) au filter huwa ni kwa lengo la kibiashara.
Hata Beyonce na Jay Z hupiga picha za faragha lakini kwa kutumia wapiga picha maalumu. Hii ni kwa lengo la kuwaonyesha mashabiki maisha yao nje ya kile wanachokifanya. Ni sehemu ya burudani. Kinachoburudisha zaidi kwenye sanaa ni upande wa pili wa maisha ya mastaa.
Solange Knowles ambaye ni mdogo wa Beyonce aliwahi kunaswa akimshambulia kwa mateke shemeji yake Jay Z. Ni tukio lililowavutia wengi duniani. Lilizungumzwa sana hasa kwa kuwa watu waliamini amani imetawala katika familia hiyo.
Famili hiyo ilitoa maelezo kwa mashabiki wao wakikiri kuwa hata wao hupatwa na mikasa kama hiyo. Ni kawaida.
Kupiga picha kihasara hasara, kutojutia pale wasanii wanapofanya makosa ni miongoni mwa mambo yanayowafanya wakose dili hizi.
Kwa mfano mwigizaji Faiza Ally alihoji sababu za kampuni ya Kedz kumpa mkataba Zari. Je, hakustahili?
Alistahili kwa sababu amejua kulitumia vyema jina lake katika raha na shida. Walipokuwa kwenye penzi zito na Diamond walishirikiana kuingiza fedha, halkadhalika katika utengano wao pia.
Pia, alistahiki kwa sababu anaishi kistaa. Anaheshimu jina lake.
Ukitazama ujumbe alioandika Zari akitangaza kuachana na Diamond unamwona mwanamke anayejua thamani ya jina lake mbele ya jamii. Inawezekana ulikuwa uamuzi mgumu kuliko lakini ilibidi ifike mwisho.
Zari anaitwa bingwa wa ‘kujiedit’, basi hata Beyonce anapaswa kuingia katika kundi hili kwa sababu hakubali kupigwa picha ovyo na anazozitoa huwa zimepita katika tanuru la kusafishwa zionekane zinavyoonekana.
Kwa hiyo ni ruksa kujiedit, ni ruksa kuweka picha za faragha zilizopigwa kitaalamu na ni sawa kwa msanii kufanya makosa ili mradi tu ayajutie.
Anayofanya watu maarufu wengi hawafanyi. Wanakurupuka kutafuta kiki na kuharibu brand zao.
Wasanii wafanye nini?
Kwanza watambue kuna fedha nyingi katika ubalozi kama wataamua kuyatumia majina yao vyema.
Hapa na pale wasanii wamewahi kupata ubalozi wa makampuni mbalimbali lakini ndoa hizo huwa hazidumu au huisha vibaya.
Makampuni na mashirika yamejaribu kujiweka na wasanii lakini umekuwa urafiki wa mashaka.
Wasanii wa Nigeria wamejitengenezea maisha katika nyanja hiyo. Hakuna msanii mkubwa asiye na mkataba wa kampuni ambao ni wa mamilioni ya fedha. Wanaendesha magari mazuri, wanamiliki majumba ya kifahari siyo kwa kutegemea sanaa peke yake bali mikataba kama hii ambayo sasa wasanii wanaanza kulialia inachukuliwa na Zari.
Kuteleza sio kuanguka. Wapo wasanii waliowahi kukumbwa na kashfa mbalimbali nchini lakini ukiwaangalia na maisha yao yalivyobadilika unaona kabisa wanajutia yaliyotokea. Muhimu ni kuonyesha kujutia na kuchukua hatua.
Kikubwa kuliko vyote ni kulinda jina na kuchangamkia fursa. Msanii anaweza kuwa na jina kubwa lakini kama hawezi kulitumia au kuzichangamkia fursa atabaki akizisoma tu kwenye magazeti kama hivi.
No comments:
Post a Comment