Saturday, March 31

Tusikubali kuwa wachuuzi wa bidhaa za wengine

Wimbo wa Tanzania ya viwanda unazidi kunoga kila kukicha.
Kwa viongozi wetu wakuu wa nchi, watendaji serikalini na wanasiasa kwa jumla, msemo wa viwanda hauwatoki midomoni kila wanapopata fursa katika majukwaa.
Kimsingi, msemo huo hauwezi kuwatoka kwa kuwa wao ndio wadau wa kwanza kama watoa dira kuelekea Tanzania ya viwanda.
Hata hivyo ili tufikie kwenye maono haya ya viongozi wetu kuhusu viwanda, tunahitaji kubadili fikra kutoka kuwa Taifa la walaji na wachuuzi hadi Taifa la waanzisha viwanda wa kutengeneza bidhaa.
Viwanda tunavyovipigia debe kuwa vijengwe kwa mamia na hata kwa maelfu kila kona ya nchi, havitatokana na wawekezaji kutoka nje pekee. Unahitajika mchango na ushiriki madhubuti wa Watanzania wenyewe katika kuanzisha viwanda vya aina mbalimbali. Na viwanda hivi havitaanzishwa kama mtazamo utaendelea kuwa uleule wa utokanao na fikra za kuwa walaji au wachuuzi pekee.
Kwa mfano, kwa nini Watanzania wengi waishie kuuza viatu na nguo? Kwa nini hatufikirii kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa hizo lhali tumejaaliwa malighafi tele?
Kwa nini Watanzania wengi waishie kuuza matunda magengeni na sokoni, lakini washindwe kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya kusindika matunda hayo wakajihakikishia tija zaidi?
Tuna mfano mzuri wa namna hivi sasa Watanzania kwa makundi wanavyochangamkia fursa kwenye kilimo, lakini wengi utakuta ama wanalima au ni wauzaji wa bidhaa zitokanazo na kilimo.
Tunachokosa ni ule uthubutu wa kuongeza thamani bidhaa hizo na mwishowe kuzipeleka sokoni kama bidhaa tofauti na ilivyokuwa awali.
Tunaamini kama Watanzania tutaukumbatia uthubutu wa kuongeza thamani bidhaa mbalimbali za kilimo na ufugaji, tutapiga hatua kubwa katika mchakato wa uanzishwaji wa aina mbalimbali za viwanda nchini.
Lakini pia tunapopiga chapuo mabadiliko haya ya kimtazamo na kifikra kwa Watanzania, hatuna budi pia kuzipa neno mamlaka husika zinazosimamia sekta ya bidhaa kama Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na mamlaka nyingine za kiserikali.
Uzoefu unaonyesha baadhi ya vyombo hivi vinarudisha nyuma juhudi za Watanzania wanaojaribu kujiongeza. Hii ni kwa sababu ya kuwapo kwa taratibu na masharti yasiyo rafiki.
Kwa mfano, leo ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuanzisha kiwando kidogo cha kusindika matunda. Anayejaribu atakumbana na mlolongo wa masharti ambayo mwishowe yatamkatisha tamaa.
Bado mamlaka zetu zina mtazamo wa kiwanda kwa kuangalia ukubwa wa ardhi anayomiliki mwekezaji, au jengo linalotumika kuzalisha bidhaa.
Ni muhali kwa mtu kuanzisha kiwanda kidogo ndani ya ua wake, kwa sababu tumejiaminisha kuwa kiwanda hakiwezi kuwa ndani ya nyumba ya mtu.
Lazima tukubali kuwa miaka 57 ya uhuru, Watanzania hatuna budi kuwa watu tunaoweza kujitafutia chakula, kukipika na kujiandalia mezani. Vinginevyo kuendelea kuwa walaji na wachuuzi wa bidhaa zinazotengenezwa na wengine, tukubali kuwa wategemezi wa kudumu wa maendeleo katika dunia hii ya ushindani.

No comments:

Post a Comment