Saturday, March 31

Mrema na kisa cha kufukuzwa uwaziri, kujiondoa CCM na alivyotimkia NCCR

Kwa vijana wa leo taarifa hizi kwao ni ngeni. Kwa waliokuwapo wakiwa na ufahamu na kumbukumbu sahihi ni zilipendwa.
Ilikuwa mwaka 1995 Tanzania ilishuhudia mtikisiko katika nyanja ya siasa, na hatimaye kuendesha Uchaguzi Mkuu wa kwanza ulioshirikisha vyama vingi vya siasa ambao ulikuwa na hamasa za kila aina.
Kabla ya uchaguzi huo, nchi na hasa Chama Cha Mapinduzi kilitikiswa na tukio hili maarufu. Ilikuwa Februari 24 pale ilipotangazwa kuwa Rais Ali Hassan Mwinyi amemtimua Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Augustino Mrema kwa kushindwa uwajibikaji wa pamoja.
Nini kilimkuta
Hatua hii ilitokana na mvutano katika Serikali ya Mwinyi, kutokana na mjadala ndani ya Bunge kuhusu ripoti ya Kamati, iliyoibua suala la mfanyabiashara wa kigeni, V. G. Chavda aliyekuwa anamiliki mashamba kadhaa ya katani nchini.
Kabla ya hapo, suala hilo lilikuwa likiandikwa sana na vyombo vya habari kwa miezi kadhaa. Kamati ya Bunge ilishauri Chavda akamatwe na kushtakiwa kwa kashfa ya kuvuja mamilioni ya shilingi.
Kamati ilimtuhumu kwa kutafuna Sh916 milioni za Mfuko wa Kubadilisha Madeni, alizokopeshwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza mashamba yake ya katani lakini hakufanya hivyo.
Baadhi ya mawaziri, isipokuwa Mrema, walikuwa wanamwona kama hana hatia. Februari 11, 1995 Serikali ilimtimua nchini. Siku tatu baadaye, Mahakama Kuu iliizuia Serikali kumtimua.
Baada ya hatua hiyo, ndipo Mrema akiwa bungeni, aliacha kukaa kwenye sehemu ya mawaziri, akakaa sehemu ya wabunge wa kawaida, alitumia fursa hiyo kuishutumu Serikali ya Mwinyi kwa kumkumbatia Chavda.
Alisema dhamiri yake ingemsuta kama angekubaliana na jinsi Serikali ilivyokuwa inaendesha suala la Chavda. Baada ya msimamo huo, Rais Mwinyi alitangaza kumtimua uwaziri kwa kushindwa uwajibikaji wa pamoja. Licha ya kwamba awali Mrema alisema asingehama CCM, baadaye alisema alikuwa ananyanyaswa na chama hicho tawala na hivyo akaamua kujivua uanachama. Siku mbili baadaye alijiunga na NCCR-Mageuzi, ambako aliyekuwa mwenyekiti, Mabere Marando alimpisha kwenye nafasi hiyo.
Katika kumbukumbu ya matukio hayo, Mrema anasema kutokana na uadilifu aliokuwa nao isingekuwa rahisi kwake kunyamazia suala la tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mkonge kwa wajanja wachache akiwamo mfanyabiashara mwenye asili ya India, V. G Chavda.
“Nchi ilikuwa inaibiwa, nilisikia uchungu sana. Nilikuwa napambana mwenyewe, haukuwa msukumo wa Serikali, ni Mrema pekee.”
Mrema anasema hata hivyo hilo halikumnyima usingizi, badala yake aliamua kupambana na kuhakikisha mfanyabiashara huyo anafikishwa katika vyombo vya dola.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mrema ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa TLP, anasema licha ya kufanya kazi vizuri akiwa CCM, siku moja aliona ni busara kukihama chama hicho na kutimkia upinzani ili aweze kutimiza kile alichokiamini.
“Siwezi kusema nilinyanyasika CCM, Rais Ali Hassan Mwinyi alikuwa ananipenda sana kutokana na utendaji wangu lakini ukweli ni kwamba watu wanaishi kwa malengo, pale nilipokuwa nimefika nisingefanya zaidi, nikajiuliza mbona nina uwezo zaidi kwa nini nang’ang’ania huku?”
“Nina marafiki wakasema kama CCM hawawezi kukupa nafasi ya kufanya zaidi kwa nini usiondoke, nikaamua kufanya maamuzi,” anasisitiza Mrema.
Uchaguzi Mkuu
Akiwa tayari NCCR-Mageuzi, Mrema aliteuliwa kuwania urais katika Uchaguzi huo wa kwanza wa vyama vingi. Alionekana kuwa na nguvu na mvuto mkubwa kwa wakati huo kutokana na kufanya kazi ya kupambana na uhalifu, rushwa, ubadhirifu na unyanyasaji wanawake alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu.
Hata hivyo, uchaguzi huo ulimalizika kwa kada wa CCM Benjamin Mkapa kuwa Rais wa Awamu ya Tatu kushinda na Mrema kuibuka katika nafasi ya pili.
Katika matokeo hayo, Mkapa alipata kura 4,026, 422 (asilimia 61.82), Mrema kura 1,808, 616 (asilimia 27.77), Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF kura 418, 973, (asilimia 6.43) na John Cheyo wa UDP, kura 258,734 (asilimia 3.97).
Wazo la urais
Mrema ambaye alijipatia umaarufu mkubwa katika uchaguzi huo na kura zake kuendelea kupungua taratibu kila alipogombea, anasema wazo la kugombea urais alilipata kutoka kwa “wapambe na washauri wake wa siasa”.
“Vijana walisema nihamie upinzani ili tusaidie nchi maana mambo yalikuwa hayaendi na wakati huo chama kilichoonyesha kunipenda kilikuwa NCCR-Mageuzi.”
“Mimi sikuwa hata na Sh100, lakini kila kitu walifanya wao ili kuhakikisha ninashinda na kuwa Rais wa Tanzania,” anasisitiza Mrema.
Hata hivyo, Mrema anasema baadaye aligundua kuwa marafiki wake hao hawakuwa na nia njema kwake, bali walitaka kumtumia kujipatia vyeo.
Mrema anasema, pamoja na kushawishiwa na marafiki hao, yeye aliamini kwamba angeweza kufanya mambo vizuri zaidi kama angekuwa Rais, kwani aliona akiwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu alishindwa kutekeleza mambo mengi kutokana na kuwa na wakubwa zaidi yake.
Mgogoro NCCR- Mageuzi
Baada ya uchaguzi huo, chama kilichomsimamisha kugombea urais, NCCR-Mageuzi, hakikupata tena utulivu. Anasema baada ya wenzake ndani ya NCCR-Mageuzi kuona ameshindwa kuwavusha katika uchaguzi na kuwapeleka ikulu, walianza maneno wakisema chama si wingi wa wafuasi huku wakitoa mifano ya vyama vingine duniani vyenye wafuasi wachache lakini vimeshinda uchaguzi.
Mrema anasema wenzake waliojenga hoja ya kuwa na chama chenye wafuasi wacache, walianza njama za kutaka kumng’oa uongozi na uanachama hali iliyosababisha NCCR-Mageuzi kuwa na migogoro ya mara kwa mara.
“Kilichotokea ni kuwa viongozi wa NCCR- Mageuzi waliamini mimi nitawavusha kwa kugawana vyeo pindi ningeshinda urais, lakini hilo halikutokea wakaanza kutengeneza visa dhidi yangu,” anasema.
Mrema anasema baada ya kuona hilo haliwezekani maadui zake wakapanga mkutano Tanga kumng’oa. Anasema kwa mujibu wa taarifa alizokuwa “amezinyaka”, maadui zake walipanga kumtoa katikati ya mkutano huo lakini ikabidi apambane ili kuhakikisha hilo halitokei.
“Niliponea chupuchupu, nilikuwa nife siku ile, hali ilikuwa mbaya ukiangalia picha huwezi amini, ilibidi nijifiche chini ya meza lakini hawakufanikisha walichotaka kwa sababu mimi ndiyo nilikuwa na nguvu,” anasema.
Mwaka 1999, Mrema alijiondoa katika chama hicho na kuutelekeza ubunge wa Temeke na kujiunga na TLP, akiwa na kundi kubwa la wanachama.
Hatua hiyo iliporomosha idadi ya wabunge wa NCCR-Mageuzi kutoka 19 iliopata 1995, hadi mmoja mwaka 2000; na kuongeza wabunge wa TLP kutoka sifuri mwaka 1995 hadi watano mwaka 2000.
Kazi anazojivunia
Mrema ambaye ndiye muasisi wa ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na sungusungu nchini, anasema kutokana na kuongezeka wa matukio ya uhalifu aliona ni bora shughuli za usalama zikawa karibu na wananchi.
“Ilikuwa creativity (ubunifu) yangu tu, lengo ilikuwa ni kusogeza huduma kwa jamii na kweli ilisaidia sana,” anasisitiza.
Mrema anasema kinachomfurahisha mpaka sasa licha ya jeshi hilo kufanya maboresho kadhaa, bado hawajapoteza lengo la msingi la vituo hivyo na kwamba vinafanya kazi vizuri.
Hata hivyo, anasema kuwa inahitajika msukumo zaidi ili kuboresha huduma katika vituo hivyo lakini pia kuendeleza majina ya waasisi kwa lengo la kuwaenzi.
‘Mfano kuna vituo vilipewa jina langu lakini leo hii ukienda vimefutwa, waliangalie hili ingawa hawapishani sana na wazo langu bado naona wanatumia mbinu zilezile. Kuhusu ulinzi wa sungusungu, Mrema anasema aligundua kuwa hata wakiwa na polisi wengi sana kila kona bila kushirikisha wananchi ni kazi bure.“Wananchi ndiyo wanalinda nchi jeshi la polisi bila ushirikiano na wananchi huwezi fanikiwa hapa ilibidi niwe mbunifu zaidi ndiyo nikaamua kutoa motisha ya Sh50,000 kwa kila kikundi kitakachofanikisha kukamata silaha au mali.”
“Nililazimisha matajiri watoe fedha na kuwalipa polisi ama vikundi hivyo vilivyokuwa vikikamata magendo; nilifanya hivyo ili kuwaongezea ari, kwani mtu anatoa maisha yake kwa sababu ya nchi, ikasababisha polisi na wananchi kuwa na moyo wa kufanya kazi.”
Usuluhishi wa ndoa
Mwenyekiti huyo wa TLP anasema katika uamuzi wake wa kusuluhisha ndoa hakukurupuka ingawa kuna baadhi ya watu walihoji iweje afanye kazi hiyo wakati siyo kiongozi wa dini.
Anasema kwa wakati huo yeye alikuwa waziri wa mambo ya ndani, wizara ambayo inashughulika na masuala ya uhalifu na kwamba wahalifu wote walikuwa chini yake.
“Mwanaume anayempiga mkewe ni sawa na mhalifu mwingine, wanawake walikuwa wanavunjwa meno, wanatelekezwa, wakifanya jambo dogo tu wanapigwa mpaka wanazimia. Ilikuwa kawaida kabisa kumnyanyasa mwanamke na jamii ikaona sawa.”
“Nilitaka kukomesha vitendo hivyo watu wasione ni kawaida. Haiwezekani, huo ni uonevu na ni uhalifu kama mwingine; siku moja nilipata taarifa kuna mama ametelekezwa na watoto na ananyanyasika, nikatoa siku saba kwamba naenda Moshi na kabla sijafika, nataka huyo mwanamme awe ameripoti. Huwezi amini yule aliyemtelekeza alipanda basi akafika kabla mimi sijafika.”
Mrema anasema hakutaka wanawake waonewe maana yeye ana mama na dada zake anaowaheshimu hivyo alitaka kila mwanamke aheshimiwe.
Anasema kutokana na tukio hilo siku moja mwaka jana alikutana na yule mama, ambaye kwa sasa ameshakuwa mzee na kuja kumkumbatia huku machozi yakimdondoka.
“Nikashangaa kwa nini mama mzee analia vile, nilikuwa simjui kwa sababu sikuwahi kumuona kwani nilisikia taarifa yake kutoka kwa mmoja wa wakuu wa mikoa, lakini mama huyo alieleza jinsi uamuzi wake ulivyoirejeshea furaha maishani mwake.
“Mama yule alisema ni mimi ndiyo nilisababisha mumewe arudi nyumbani na kusomesha watoto wake na sasa watoto hao wanafanya shughuli na kupata kipato cha kumlea yeye na baba yao, lakini pia mumewe alirudi na kumuhudumia kama kawaida kwa kumuhofia Mrema.”
Kama kawaida yake, Mrema haachi kutamba, anasema ulifika wakati alikuwa akijulikana kuliko hata baadhi ya mawaziri kwa utendaji wake wa kazi jambo lililompa nguvu na ari ya kufanya kazi zaidi.
“Kuna kitu siwezi kukisahau maishani mwangu, nakumbuka siku moja Rais Mwinyi alikwenda kikazi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na aliporejea aliniita ofisini kwake kisha kunipa salamu zangu kutoka kwa wananchi wa huko.
“Nilishangaa sana, yaani Rais anatembelea eneo na kutatua mambo mengi, lakini inafika mahali anasimamishwa na wananchi kisha wanamwambia aje anisalimie. Hii iliniongezea ari ya kufanya kazi zaidi kwani ilionyesha wazi wananchi wana imani na mimi.”

No comments:

Post a Comment