Maafisa wa forodha katika uwanja mmoja wa ndege nchini China wa walipigwa na butwaa walipofungua mkoba wa wanandoa wawili na kugundua kwamba ulikuwa umejaa mende.
Kwa mujibu wa gazeti la Beijing Youth Daily maafisa katika uwanja wa ndege wa Baiyun kusini mwa Guangdong waligundua kulikuwa na viumbe waliokuwa wanatembea walipoweka mikoba ya wawili hao kwenye mtambo wa x-ray wa kukagua mizigo.
"Kulikuwa na mfuko wa plastiki wa rangi nyeupe na ndani kulikuwa na vitu vya rangi nyeusi vilivyokuwa vinatambaa," afisa mmoja wa usalama kwa jina Xu Yuyu aliambia Kankan News.
"Mmoja wa wafanyakazi aliufungua mkoba huo na mende wengi wakatoka na kuanza kutambaa. Karibu alie," alisema Bi Xu.
Walipoulizwa ni kwa nini walikuwa wanawasafirisha mende hao, mwanamume huyo alisema ni wa kutumiwa kama dawa ya kuchua ngozi ya mke wake.
Hakufafanua ni tatizo gani la ngozi linamsumbua mke wake, lakini Bi Yu anasema maafisa walifahamishwa kwamba: "Ni sehemu ya tiba ya jabi. Unawachanganya mende na mafuta fulani na kujipaka kwenye ngozi.
Gazeti la Beijing Youth Daily linasema viumbe walio hai huwa hawaruhusiwi kubebwa kama mizigo ndani ya ndege na kwa hivyo wawili hao walitakiwa kuwaacha na maafisa wa usalama uwanja wa ndege.
Haijabainika mende hao walifanyiwa nini baadaye.
Hii si mara ya kwanza kwa maafisa wa usalama uwanja wa ndege kupata vitu vya kushangaza wakikagua mizigo.
Agosti, maafisa waligundua mwanamume mmoja aliyekuwa anasafirisha mikono miwili ya binadamu.
No comments:
Post a Comment