TBA imechelewa kuanza ubomoaji wa jengo hilo baada ya Tanesco kuomba waondoe wenyewe madirisha, milango na AC, kazi ambayo amepewa kuifanya mpaka leo Ijumaa jioni kabla ya ubomoaji kuanza.
Akizungumza na gazeti hili leo Ijumaa wakati uondoaji wa madirisha ukiendelea, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Mhandisi Elius Mwakalinga amesema kazi waliyonayo ni kubwa lakini wamejipanga kuikamilisha kwa wakati.
"Mpaka sasa hatujapata mchoro wa jengo hili baada ya kujengwa, tunachofanya ni kupima na kuchora ili kuepusha madhara. Unaweza ukakata bomba la gesi hapa ikawa shida tena," amesema Mwakalinga.
Amesema suala kubwa wanalolizingatia kwenye ubomoaji huo ni usalama na kwamba watatoa mafunzo maalumu kwa wafanyakazi kuhusu kujikinga wakati kazi hiyo ikiendelea.
Amebainisha kwamba watabomoa jengo la mbele pekee bila kuathiri lile la nyuma. Hata hivyo, amekiri kwamba jengo litakalobaki litakosa mwonekano mzuri kwa sababu sehemu ya mbele inayobeba sura ya jengo itakuwa imeondolewa.
"Tutatumia teknolojia mbili katika kubomoa jengo hili ambazo ni manual na mechanical. Tungeweza kutumia njia ya kulipua lakini tumeona itaathiri shughuli nyingine za kiuchumi," amesema.
Mwakalinga amesema athari zitakazojitokeza wakati wa ubomoaji ni kelele pamoja na vumbi. Amesema wamefanya tathmini ya jengo na kuangalia athari za mazingira na kujiridhisha kwamba ni chache.
Kuhusu gharama za ubomoaji, Mwakalinga amebainisha kwamba bado hawajakubaliana kuhusu hilo lakini watakaa na Tanesco kuzungumza kuhusu gharama hizo.
"Sheria ya manunuzi ya umma inasema ukishampa mtu kazi bila kutangaza tenda mnapata fursa ya kukaa na kujadili gharama wakati kazi inaendelea. Kwa hiyo, tutakaa na kuzungumzia hilo, hii ni taasisi ya umma na agizo limetoka kwa Rais," amesema Mwakalinga.
No comments:
Post a Comment