Friday, December 1

Seneta afutiwa shahada ya sheria kwa kudanganya


Nairobi, Kenya. Chuo Kikuu cha Nairobi kimefuta cheti cha shahada ya sheria ya Seneta wa Meru, Mithika Linturi kwa tuhuma za kutumia stakabadhi bandia kusajiliwa katika chuo hicho.
Uamuzi huo uliafikiwa na Baraza Kuu la chuo hicho baada ya kufanya uchunguzi wa kina kwa ushirikiano na Tume ya Elimu ya Juu kuhusu uhalali wa stakabadhi alizotumia seneta huyo kusomea sheria katika chuo hicho.
Hata hivyo, seneta huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa chuo hicho umechochewa kisiasa na kwamba alitumia vilelezo sahihi kusajiliwa chuoni hapo.
Hii si mara ya kwanza kwa Linturi kupata pigo kuhusu elimu yake kwani wiki moja iliyopita Jaji wa Mahakama ya Juu mjini Meru, Ann Ong’injo aliagiza tume ya uchaguzi pamoja na ofisa aliyesimamia uchaguzi eneo hilo, Samuel Gichichi kuwasilisha nakala za vyeti halali vya elimu vya seneta huyo. Hatua hiyo ilikuja baada ya  Mugambi Imanyara kupinga kortini ushindi wa Linturi kama Seneta wa Meru.
Linturi alikuwa miongoni mwa wanasiasa 106 waliokuwa wanachunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC)kwa madai ya kikiuka kipengele cha maadili katika katiba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.

No comments:

Post a Comment