Monday, October 16

Ukweli kuhusu njaa unauma sana

Ukweli unaohusiana na kitisho cha njaa miongoni mwa familia nyingi barani Afrika ni jambo linalouma sana, hasa inapozingatiwa kwamba hili ni bara lenye ardhi kubwa yenye rutuba, sambamba na rasilimali kadhaa.

Somalia Mogadischu | unterernährtes Kleinkind (DW/S. Petersmann)
Ni moja  ya matukio au hali kama hizi ambapo mtu hugunduwa kile hasa kinachotokea. Daktari na muuguzi wanaanza kumpatia matibabu na kumrejeshea pumzi mtoto mdogo. Mzazi ameduwaa pembezoni mwa kitanda.
Baada ya dakika chache, daktari anamtaka muuguzi asitishe jaribio lake. Kimya kinatawala. Baada ya hapo inasikika sauti ya kilio. Muuguzi anachukua chombo kimoja na kukiweka pembeni mwa kitanda cha hospitali. Hapo tena hatuoni kinachoendelea.
Tukio hili  katika zahanati moja kaskazini mwa Kenya, ni mojawapo ya hali za kuhuzunisha sana kuhusu utafiti wetu juu ya janga la njaa barani Afrika.
Inaonesha kwamba watu milioni 26 wanaokabiliwa na njaa si watu wenye kutiliwa maanani na ni wazi kwamba kinachowakabili baadhi yao ni zaidi na kitisho.  
Somalia Mogadischu | unterernährtes Kleinkind (DW/S. Petersmann)
Watoto nchini Somalia walio na ugonjwa wa utapiamlo
Msichana huyo mdogo katika zahanati hiyo nchini Kenya hakufariki dunia kwa sababu ya ugonjwa usiotibika au kutokana na ajali, lakini alifariki kwa sababu hakula kitu kwa muda mrefu.
Njaa si suala linalogonga vichwa vya habari

Kwa wiki kadhaa, waandishi habari wa Deutsche Welle wamekua wakifuatilia mzozo wa njaa barani Afrika. Wamezungumza na wasaidizi, wataalamu, wanasiasa na zaidi ya yote wahusika, ili kupata zaidi juu ya sababu ya watu wengi kuwa katika hali ya njaa.
Wakati wa kufanyika mradi huu si jambo la nadra. Tayari kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, mashirika ya msaada yamekuwa yakitoa tahadhari kubwa kwamba hali mbaya kabisa ya ukame kuwahi kuonekana katika miongo ya karibu inaweza kuzuka barani Afrika na Yemen.
Lakini muda si mrefu baada ya hapo,  mzozo huo haukutiliwa maanani katika vichwa vya habari, licha ya kwamba hali leo bado haijaboreka . Katika nchi mbili zilizoathirika zaidi, Sudan Kusini na Somalia, zaidi ya  watu milioni 14 bado wanategemea msaada wa chakula.
Sababu ni binaadamu 
Nini kimesababisha hali hii? Jibu la mwandishi ni wazi: Sio maumbile lakini binadamu.
Mabadiliko ya tabia nchi duniani, ukataji miti mkubwa na kutumiwa kwa ardhi na kundi fulani tu la watu kunawafanya wadau wadogo wadogo kuzidi kukabiliwa na ugumu wa maisha.
Hunger in Somalia (picture-alliance/Photoshot)
Njaa nchini Somalia, wananchi wakipatiwa chakula cha msaada
Lakini mbali na hayo, migogoro ya kisiasa inasababisha uharibifu mkubwa zaidi. Nchi zinazoathirika zaidi ni kuanzia Nigeria hadi Sudan Kusini mpaka Somalia - ama  kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe au makundi ya kigaidi ambayo yanalifanya eneo zima kuwa lisilokuwa na usalama. Huduma ya afya, elimu au usalama ni sawa na kuwa neno la kigeni kwa raia wengi. Badala  yake kikundi kidogo cha watu kinajitajirisha  na mara nyingi kwa utajiri mkubwa.
Matumaini ya shaka shaka
Pamoja na hayo, kikundi cha waandishi habari kimerejea na ripoti za matumaini. Kwa mfano, Somalia ina serikali mpya tangu mwanzoni mwa mwaka baada ya zaidi ya  miaka 20 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Watazamaji wengi angalau wana matumaini yenye shaka shaka - na kila mahala waandishi walikutana na watu walio katika mazingira ya kipekee, lakini hawakukata tamaa.
Binadamu sio tu ndiye sababu wa  janga la njaa, lakini pia ndiye suluhisho. Zaidi kuhusu njaa barani Afrika kuanzia tarehe 16 Oktoba, sikiliza matangazo yetu ya Deutsche Welle kila siku kwenye anwani: www.dw.com.
Mwandishi: Jan-Phillip Scholz
Tafsiri: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Iddi Ssessanga

No comments:

Post a Comment