Monday, October 16

Makamu wa Rais akemea tochi kugeuzwa chanzo cha rushwa


Moshi. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaonya askari wa kikosi cha usalama barabarani kutogeuza tochi kuwa chanzo cha kudai rushwa.
Pia, amewataka kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Kwa upande wa madereva amewataka kuwaona askari kuwa ni walinzi wao.
Amesema hayo leo Jumatatu katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani uliofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro katika viwanja vya Mashujaa mjini Moshi.
Samia amesema takriban asilimia 76 ya ajali za barabarani husababishwa na makosa ya kibinadamu kutokana na utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari, uchovu wa madereva na ulevi.
Amesema sababu nyingine zinazochangia ajali za barabarani ni miundombinu mibovu ya barabara inayochangia kwa asilimia nane na ubovu wa magari unaochangia kwa asilimia 16.
Makamu wa Rais amesema idadi kubwa ya ajali hizo zinasababishwa na uzembe wa waendesha bodaboda ambao unaweza kuepukika.
Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.
“Mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” amesema.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21.
Samia ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia 33.
Ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Ameyataja makosa hayo kuwa ni mwendo kasi, ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutovaa mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wakiwa ndani ya gari.
Makamu wa Rais amewataka kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wote kupitia taasisi mbalimbali, kujipanga na kuhakikisha wanabadilishana uzoefu wa namna ya kukabiliana na tatizo la ajali.
Amewataka kutoa machapisho yenye kutoa elimu kwa makundi yote ya watumiaji wa barabara na kusimamia mafunzo ya umahiri wa uendeshaji wa vyombo vya moto.
Pia, amewataka askari wa usalama barabarani kufanya doria za mara kwa mara katika barabara kuu na za ndani ili kudhibiti makosa ya usalama barabarani na ajali zisizo za lazima.
Kwa upande wa abiria amewataka kuwa makini na kujenga tabia ya kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria za usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment