Tuesday, July 18

RC RUKWA AITAHADHARISHA MANISPAA YA SUMBAWANGA KUTUMIA VIZURI BILIONI 1.1 ZA UKARABATI KANTALAMBA


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amewataka wale wote wanaohusika na usimamizi wa fedha za ukarabati wa moja ya shule Kongwe nchini, kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.

Ameyasema hayo baada ya kuzungukia maeneo yote ya shule yanayoendelea kukarabatiwa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza ili kujionea hatua waliyofikia katika ujenzi na kutathmini kama thamani ya pesa inakwenda sambamba na ujenzi unaoendelea katika shule hiyo.

Shule ya Sekondari ya Kantalamba ni miongoni mwa shule kongwe 20 nchini ambazo serikali kupitia Wizara ya Elimu imeweka mpango wa kukarabati shule hizo kwa lengo la kutunza hadhi na kuziboresha zaidi. Ambapo shule hiyo imepata mgawo wa shilingi 1,123,353,700/=
“Tafadhalini sana Mwalimu Mkuu, Mkurugenzi, Afisa Elimu na sisi wote tuhakikishe kwamba shule hii imebadilika kwa kuwa hizi pesa si kidogo, bilioni sio hela kidogo, zisichezewe, zifanye kazi iliyokususdiwa na kazi yenyewe ioneshe sura ya bilioni, isijekutokea tukapata kazi nyingine ya kusema kwamba hizi pesa kazi iliyofanyika ni ya hovyo hovyo,” Mh. Zelote Alisisitiza.


Baada ya kuona juhudi zinazoendelea katika ukatabati huo Mh. Zelote amesifu uongozi wa shule wa kuajiri mafundi vijana waliopo mtaani ili kuwa na matumizi mazuri ya fedha hizo tofauti na kuwatumia wakandarasi ambao wangesababisha fedha nyingine zipotee bila ya sababu, na kusisitiza kuwa vijana hao wasimamiwe kwa ukaribu sana na kupewa maelekezo ili wasilipue kazi inayoendelea.  

Pamoja na hayo Mh. Zelote alilisisitiza uwazi kwenye matumizi ya fedha za umma, na kuwataka wakaguzi kuwa makini na kukagua kila hatua ya ujenzi na kuona kuwa kila senti inayotumika inaendana na thamani ya ujenzi inayoonekana. Aidha alizitaka Halmashauri zote Mkoani Rukwa kutenga bajeti kwa kupitia mapato yake ya  ndani ili kuboresha miundombinu ya shule jambo ambalo linaweza kubadilisha muonekano wa shule nyingi mkoani humo.
“Ningependa kuona shule hii inakuwa ya mfano kwakuwa ipo katika makao makuu ya mkoa na pia alishauri kujenga uzio na kuendeleza utunzaji wa mazingira kwa kuweka sharia kali kwa wanafunzi ili waendelee kutunza mazingira ya shule,” Mh. Zelote aliongezea.  

Awali alipokuwa akisoma taarifa fupi ya ukarabati wa shule kongwe Sekondari ya Kantalamba mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Martin Kasansa alitaja changamoto kadhaa zinazorudisha nyuma kasi ya ukarabati wa shule hiyo ikiwemo uchakavu mkubwa wa bwalo uliosababisha kuanza upya ujenzi, upatikanaji wa baadhi ya vifaa mkoani Rukwa kuwa mgumu na kulazimika kuagiza kutoka mkoa wa Mbeya na kutopatikana kwa maji kumechelewesha ujenzi unaoendelea.  

“Kazi ya ukarabati ilianza rasmi mwezi June 2017 na inasimamiwa na mwandisi kutoka Chuo cha Sayansi na teknolojia Mbeya na inategemewa kumalika ndani ya miezi mitatu, lakini upatikanaji wa maji umekuwa ni tatizo katika eneo letu, ” Martin Alisema.
Ukarabati unaoendelea katika shule hiyo unahusisha mabweni 6, vyumba vya madarasa 14, ofisi za walimu, vyoo, mfumo wa maji safi na maji taka, mfumo wa umeme, jiko, bwalo, maabara pamoja na jingo la kilimo. Ambapo mapaka sasa Shilingi 648,051,540.90/= imeshatumika na kufikia asilimia Zaidi ya 58.

Nae Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bernard Makali aliutaka uongozi wa shule kuangalia maeneo muhimu na kuweaza kuyamalizia ili wanafunzi wasiachwe nyuma na muhula wa mwaka huu na kusisitiza kuwa upishi wa kutumia kuni si mzuri na kuahidi kushikiana nao kutafuta namna ya kupikia kwa kutumia gesi jambo ambalo litatunza mazingira.

No comments:

Post a Comment