Tuesday, July 18

RC MAKONDA ATOA SIKU SABA KUHAKIKISHA WIZI WA VIFAA VYA MAGARI UNAKOMESHWA MARA MOJA


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda leo ametoa siku saba kwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam DCP Lucas Mkondya kuhakikisha wizi wa vifaa vya Magari unakomeshwa mara moja.

Akitoa maagizo hayo, Mheshimiwa Makonda amesema wizi wa vifaa vya magari vikiwemo Vioo, Radio, Side mirrow, Power Window,Taa pamoja na Shoo ya mbele na nyuma ya Gari vimekuwa vikishamiri kila kukicha jambo linalowakera wananchi na kuwapa hofu ya kuweka magari yao kwenye maegesho kwa kuhofia kuibiwa kitendo ambacho amesema hakivumiliki.

“Sitaki kusikia watu wanaibiwa vifaa vya Magari yao,watu wanaibiwa Vioo, Power Window,Radio, Taa,Side Mirror na wakati mwingine wanavunja vioo vya gari na kuiba Pochi na Laptop, sasa haiwezekani wizi wa namna hii uendelee kwenye Mkoa  wangu, sasa Kaimu Kamanda Kanda Maalumu nakuagiza na ninakupa siku saba sitaki kusikia wizi wa vifaa vya magari ukiendelea, nataka ifikie hatua mtu aweze kuegesha Gari lake na kulikuta likiwa salama” Alisema Makonda.

“Mwananchi yoyote atakaeibiwa na akapeleka taarifa Polisi na hatua za kisheria zichukuliwe atoe taarifa kwangu bahati nzuri wananchi wana namba zangu, haiwezekani Mwananchi anajikusanya na kununua gari alafu anaibiwa watu wanaiba vifaa vyake, wizi wa namna hii nasema Mwisho ndio umefika leo," Alisisitiza Makonda.

Aidha Makonda ameagiza Maduka na Vijiwe vyote vinavyouza vifaa vya Magari kujisajili mara moja iliviweze kutambulika na Serikali.“Kinachoshangaza ni kwamba hawa wanaoiba wana vijiwe vyao ambapo wanauza hivyo vifaa, ukienda Kariakoo, Magomeni na pia Temeke (Keko) kuna vijiwe ambavyo ukienda kule unakuta kifaa kilichoibiwa kwenye Gari lako kipo mtaani kinauzwa” Aliongeza Makonda.

Akipokea Maagizo hayo, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam  DCP Lucas Mkondya amesema kuwa maagizo hayo yanaanza kutekelezwa leo ambapo msako utaanza leo kuhakikisha Genge la wezi wa vifaa vya magari vinasambaratishwa.

Aidha amewaagiza Makamanda wa polisi Temeke, Ilala na Kinondoni kuanza utekelezaji wa maagizo hayo kuanzia leo na kuwataka wote wanaouza vifaa vya wizi kujisalimisha mara moja kwa Jeshi la Polisi.

No comments:

Post a Comment