Akizungumza leo Jumanne, Julai 18 wakati wa operesheni hiyo maalum ya kufanya ukaguzi wa nyumba kwa nyumba kwenye kitongoji hicho, Kamishina wa Intelijensia wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Fredrick Kibute, amesema wamefanikiwa kukamata dawa hizo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Amesema walituma kikosi kazi cha watu wachache kuchunguza uwepo wa taarifa hizo.
“Baada ya kujiridhisha na taarifa hizo, tulianza safari kutoka Dar es salaam na juzi usiku wa manane tulianza upekuzi na kukamata magunia hayo 428,"amesema Kamishna huyo.
Amesema walikamata magunia 428 ya bangi usiku huo na magunia sita ya mbegu za bangi ambazo zilikuwa zimefichwa ndani.
"Lilikuwa jambo la kushangaza usiku huo hatukukuta watu ndani ya nyumba ingawa zilikuwa wazi, baadhi ya nyumba zilikuwa zimefungwa, zilizofungwa tuliamua kuchukua uamuzi wa kuvunja na tulikuta kila nyumba ina bangi," amesema.
Kamishna Kibute amesema pia licha ya eneo hilo kuwa mbali limesababisha viongozi wengi kushindwa kufika maeneo hayo kwa ajili ya ukaguzi.
"Huku ni mbali hasa ukiangalia ni eneo wanaloishi watu wachache, kikubwa tunaomba ushirikiano zaidi kutoka kwa wananchi juu ya uwepo wa madawa hayo kwenye maeneo hayo," amesema.
Kamishna Kibute aliwataka wananchi wa wilaya ya Arumeru kuacha mara moja biashara ya kilimo cha bangi kwa kuwa serikali ya awamu ya tano si mchezo na kuwataka watambue kuwa hawapo salama na atahakikisha anakomesha kilimo haramu cha biashara ya dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment