Tuesday, July 18

BANK OF AFRICA YAKABIDHI GREDA KWA MTEJA WAKE


BANK OF AFRICA imekabidhi rasmi mtambo wa ujenzi (Greda jipya aina ya JCB) lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300 kwa kampuni ya Dezo Civil Contactors Limited, kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi ikiwemo kandarasi ya ujenzi wa kuta kwenye Pwani ya Bahari ya Hindi. 

Makabidhiano ya mtambo huu ni sehemu ya mpango endelevu wa benki wa kununua na kukodisha mitambo (lease finance), ambayo inawawezesha wateja kujiongeza kiutendaji kwa kupata vifaa vya kisasa bila ya kulazimika kuwa na pesa taslimu za manunuzi ya vifaa hivyo. 

Makubaliano haya ya ukodishaji wa mitambo yanaakisi katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi, usafirishaji, teknolojia ya habari na mawasiliano, utalii, madini, mafuta na gesi.

BANK OF AFRICA imebaini huu ni mpango ambao una tija kubwa kwa wajasiriamali wakubwa kwa wadogo, kwa ajili ya kufanikisha uendeshaji wa biashara zao ambao utaongeza uzalishaji na faida kubwa. Mteja kupitia mpango huu anapewa fursa pana ya kufanya chaguo lake bila kikwazo chochote na bila ya uhitaji wa amana ya awali au dhamana nyingine. Marejesho ni malipo ya ukodishaji ya kila mwezi na mteja ana uwezo wa kuchagua kua mmiliki wa mali husika pindi ifikapo mwisho wa mkataba wa ukodishaji. 

Benki humsaidia mteja kuhakiki chombo anachotaka kuingianacho mkataba kama kina ubora ili kuweza kuinua uchumi wake na uchumi wataifa kwa ujumla.
Naibu Mkurugenzi mtendaji wa BANK OF AFRICA TANZANIA Bw. Wasia Mushi akikabidhi mfano wa funguo kuashiria makabidhiano ya Greda kwa Mteja Bw. T Hitesh Vishram ambae ni Project Supervisor wa Kampuni ya Dezo Civil Contractors Limited, Katikati ni meneja wa masoko, Utafiti na maendeleo wa BANK OF AFRICA TANZANIA Bw. Muganyizi Bisheko.

No comments:

Post a Comment