Tuesday, April 10

Samia atia neno wanawake ‘waliotelekezwa’


Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuibuka na kampeni ya kuwasaidia wanawake wenye watoto ‘waliotelekezwa’.
Mbali na kumpongeza mkuu huyo wa mkoa, amewataka wanaume waliowazalisha wanawake hao iwe kwa kupenda au bahati mbaya kuchukua jukumu la malezi ya watoto wao.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 10, 2018 wakati akizindua chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 uliofanyika leo katika viwanja vya Mbagala Zakeem jijini.
Samia ametoa kauli hiyo baada ya awali Makonda kumueleza kuhusu kampeni hiyo sambamba na idadi ya watu waliotajwa kuzaa na wanawake hao na kuwatelekeza, wakiwemo wabunge na viongozi wa dini.
Makamu wa Rais ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kumuunga mkono kiongozi huyo katika jitihada alizozianza kuokoa kinamama na watoto.
Aidha aliwataja wahusika wakiwemo wanasheria na vituo mbalimbali vinavyohusika na masuala ya ustawi wa jamii kupitisha suala hilo katika njia sahihi kisheria, huku akiwataka Watanzania kuunga mkono na si kukosoa juhudi hizo.
"Mkuu wa mkoa nakupongeza, hatua hii itatupa takwimu zitakazosaidia kufanya utafiti, pengine na mikoa mingine itafanya, naomba baada ya hatua hii wakina mama hawa waelekezwe njia za kufanya," amesema.
"Taasisi nyingine nazo zitoe ushirikiano, tukikosoa hatua hizi za awali tutakuwa hatusaidii jamii, maofisa maendeleo jamii wapo pale baada ya hatua hii wayabebe yatakayokusanywa, watakaokubaliana yaishe wayamalize lakini yale yatakayopelekwa mahakamani yapelekwe."

No comments:

Post a Comment