Mashambulizi ya makombora yamepiga katika kambi ya jeshi la Syria leo (09.04.2018) lakini Marekani na Ufaransa zinakanusha kuhusika kama hatua ya kujibu shambulizi la gesi ya sumu lililofanywa Jumamosi mjini Douma.
Shirika la habari la serikali ya Syria SANA limeripoti mapema leo alfajiri kwamba makombora kadhaa yamevurumishwa katika kambi ya jeshi ya Tiyas katika mkoa wa kati wa Homs. Shirika hilo limesema mifumo ya ulinzi wa anga imeanza kutumika na awali liliripoti kuhusu shambulizi linaloshukiwa kufanywa na Marekani, lakini baadaye likafuta kabisa kuitaja Marekani.
Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria limesema wapiganaji 14 wameuawa, wakiwemo wanajeshi wa Iran wanaouunga mkono utawala wa rais wa Syria, Bashar al Assad.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, amekanusha madai ya Marekani kuhusika na shambulizi hilo, lakini akasema wanaendelea kuifuatilia kwa karibu hali nchini Syria na itaendelea kusaidia juhudi za kidiplomasia zinazofanywa kuwawajibisha waliohusika na shambulizi la sumu katika mji uliozingirwa wa Douma huko Ghouta Mashariki, siku ya Jumamosi ambapo watu 40 waliuawa.
Shambulizi lakosolewa vikali
Rais wa Marekani, Donald Trump, na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, hapo jana walilaani vikali shambulizi hilo la sumu na kuapa kuchukua hatua za pamoja kujibu shambulizi hilo ambalo limeibua wasiwasi kote ulimwenguni na kukosolewa vikali. Trump alisema rais wa Urusi, Vladimir Putin, Urusi na Iran wanahusika aktika kumuunga mkono mnyama Bashar al Assad na akaonya watalipa kwa gharama kubwa.
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema hakuna kinachoweza kulihalalisha shambulizi la sumu nchini Syria wakati alipokuwa akiifunga misa jana Jumapili. Alizungumzia taarifa za kutisha za watu kuuliwa katika mashambulizi ya mabomu yanayosababisha majeruhi wengi, miongoni mwao watoto na wanawake.
"Tuwaombee waliokufa, majeruhi na familia za wahanga ambazo zinateseka. Hakuna vita vizuri wala vibaya, na hakuna kinachoweza kuhalalisha nyenzo za maangamizi ya namna hii zinazowaua watu wasioweza kujilinda. Tuwaombee wanasiasa na viongozi wa kijeshi wachague njia nyingine ya mazungumzo, ambayo pekee inaweza kuleta amani badala ya kifo na maangamizi."
Rais wa Uturuki Recep Tayaip Erdogan amelilaani vikali shambulizi hilo la sumu huko Douma akizituhumu nchi za Magharibi kwa kuupuzilia mbali siasa chafu za kinyama zinazoendeshwa na utawala wa Syria. Akizunguza mjini Siirt, Erdogan alisema umma wa Uturuki haukubaliani kabisa na mwenendo huo.
"Tunapinga kwa nguvu zote undumakuwili huu na siasa hizi za kinyama. Nchi za Magharibi! Ni lini mtakapogeuka na kuwatazama watoto hawa, wanawake hawa wanaouliwa Ghouta Mashariki ili tuseme mnatenda haki?"
Kikao cha baraza la usalama kufanyika
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuijadili hali nchini Syria huku Umoja wa Ulaya ukisema ushahidi wote wa shambulizi la sumu unaashiria limefanywa na utawala wa Syria. Iran kwa upande wake imesema shambulizi hilo linatumiwa kama kisingio cha kufanya harakati ya kijeshi Syria.
China imesema leo inaunga mkono uchunguzi kuhusiana na shambulizi linaloshukiwa kuwa la sumu mjini Douma huku ikitoa wito kwa baraza la usalama na shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za sumu OPCW kuendelea na jukumu lao kama wadau wakuu wa kulishughulikia tatizo hilo.
No comments:
Post a Comment