Tuesday, April 10

Mwanaume apeleka malalamiko ya kunyanyaswa na mke

Dar es Salaam. Mkazi wa Kitunda, Mohammed Juma ametinga katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akidai kunyanyaswa na mke wake.
Akizungumza na MCL Digital leo Aprili 10, Juma amesema amefukuzwa na mke wake katika nyumba ya urithi, kisha mwanamke huyo kuwafukuza wazazi wake na watoto wa Juma.
“Wanaume tuna matatizo mengi lakini hatuyasemi, hatuyazungumzi bayana, imefikia wakati tupate nafasi tutoe manung’uniko yetu,” amesema.
Amesema wanawake wana umoja ndiyo maana wanaweza kusema matatizo yao, lakini wanaume nao wanafanyiwa mambo ya ajabu lakini wanavumilia kwa kuwa hawana pa kusemea.
“Nimejenga nyumba kwa fedha zangu, kwa sababu nafanya kazi kwa Wahindi, lakini mwanamke amenidhulumu na akafikia hatua ya kuwafukuza wazazi wangu na watoto wake wa kufikia,” amesema.
Wake kwa waume wamefurika katika ofisi ya Makonda leo baada ya mkuu huyo wa mkoa kuagiza wenza waliotelekezwa na kuachiwa watoto, wafike ili wapewe msaada wa kisheria.

No comments:

Post a Comment