Tuesday, April 10

Mtoto aliyemzuia baba’ke kuuza shamba apokewa kifalme shuleni

Mwanga. Mtoto Anthony Petro (10) wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera aliyemzuia baba yake kuuza shamba, amepokewa kama mfalme wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya kuwasili katika Shule ya Amani Vumwe kwa ajili ya kuanza masomo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mwanga, Golden Ally Mgonzo alimvisha Anthony mataji ya maua kuonyesha upendo na jinsi wananchi wa wilaya hiyo walivyopendezwa na ujasiri wake kama mkombozi wa familia.
Pia aliimbiwa nyimbo za kumkaribisha akiitwa mtoto shujaa toka wilayani Ngara.
Katika mapokezi hayo wanafunzi wa shule hiyo, viongozi mbalimbali wa halmashauri ya Mwanga na Ngara na wananchi waliotamani kumuona walikuwwepo. Mgonzo alimuombea Anthony amani na upendo pamoja na baraka awe kiongozi bora ndani na nje ya Tanzania
Alisema mtoto huyo amekuwa na ujasiri, utii, heshima, juhudi na kazi ukiwemo ushirikiano katika kupigania haki za familia bila kutumia ubinafsi na uchoyo.
“Tutahakikisha kipaji chake kinalindwa kwa weledi na kuelekeza kile kitakachokuwa matamanio ya maisha kwake,” alisema.
Ofisa elimu msingi wa wilayani Mwanga, Allan Saidi alisema mtoto huyo ameachwa na waliompeleka na atakuwa katika mazingira salama ili aweze kusoma vizuri na kutimiza malengo yake.
Alisema idara yake itakuwa ikiratibu maendeleo ya taaluma na mahitaji yake kama yataweza kupungua halmashauri kupitia idara hiyo itawajibika kusaidia.
Katika hatua nyingine, ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngara, Mussa Balagondoza alimkabidhi Anthony kwa ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mwanga, Alex Kameo akidai mtoto huyo hana kovu wala jeraha, hivyo atunzwe na kuangaliwa kwa ukaribu.
“Tunashukuru waliomuibua na vyombo vya habari kufuatilia na kuufahamisha umma kuhusu familia ya mtoto huyu, kiujumla anatoka kaya maskini ambayo hata sisi maofisa ustawi tusingejua kama si vyombo vya habari kushiriki,” alisema.
Anthony aliwatoa machozi waliohudhuria hafla ya mapokezi aliposimama na kusimulia kisa cha kutaka kumshtaki polisi baba yake aliyetaka kuuza shamba.
Akizungumzia ujio wa Anthony, meneja wa Shule ya Amani Vumwe, Isihaka Msuya alisema alimjua kupitia mitandao ya kijamii na kuguswa na maisha yake, hatimaye kuandika kuwa atamsomesha hadi mwisho mwa ndoto zake.

No comments:

Post a Comment