Friday, April 6

Dk Abbas awapa ushauri wasomi


Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas  amewataka vijana, hasa wasomi wa fani mbalimbali kutumia elimu yao kwa maendeleo ya Taifa.
Amesema badala ya kutumia elimu hiyo kushinda mitandaoni kutukana Serikali, waitumie kwa manufaa ya wengi.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 6, 2018 wakati wa uzinduzi wa kitabu cha ‘Uchumi wa viwanda’ Dk Abbas amesema kitabu hicho kimeandikwa wakati ambao nchi inahitaji uelewa mpana wa masuala ya viwanda.
"Huyu ni mhandisi muda huu angekuwa mitandaoni akiitukana Serikali yake au akiunga mabomba, lakini ametumia akili aliyonayo kutunga kitabu. Kitabu hiki kimeandikwa katika lugha rahisi na kimejaribu kuainisha aina za viwanda na umuhimu wa kuwa navyo,” amesema Dk Abbas.
Mkurugenzi huyo wa Idara ya Habari Maelezo amesema katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, nchi ina viwanda 3,306.
Mtunzi wa kitabu hicho, mhandisi  Yuda Kemincha amesema ametunga kitabu hicho kuainisha aina za viwanda na namna ya kuvianzisha na kuviendeleza.
Amesema hakuna kinachoweza kuwaokoa vijana zaidi ya kusoma, kutambua kitu kwa undani na kukifanyia kazi.
"Nimejaribu kuainisha aina za viwanda hususani kwa wenye mitaji midogo na jinsi ya kuviendeleza.
"Lengo langu ni kuona hakuna anayebaki nyuma katika uchumi wa viwanda bila kujali ana kipato kikubwa au kidogo kiasi gani, nimetumia lugha rahisi ambayo kila mmoja ataielewa" alisema Mhandisi Yuda.

No comments:

Post a Comment