Friday, April 6

Bakwata yafanya mageuzi makubwa ya uendeshaji


Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limefanya mageuzi makubwa katika mfumo wake wa uendeshaji ikiwamo upatikanaji wa masheikh wa kata, wilaya na mikoa.
Akitangaza mageuzi hayo katika mkutano na wanahabari jana, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata, Sheikh Khamis Mataka alisema mkutano mkuu wa baraza hilo uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma uliazimia kufuta utaratibu wa uchaguzi wa masheikh sambamba na maimamu wa misikiti.
Sheikh Mataka, alisema sasa viongozi hao watakuwa wakiteuliwa na Baraza la Ulamaa ambalo litawateua masheikh wa mikoa na wilaya na masheikh wa kata watateuliwa na mabaraza ya masheikh ya mikoa, huku maimamu wa misikiti wakiteuliwa na baraza la masheikh la wilaya.
Sheikh Mataka alisema ili kukabiliana na hali yoyote inayoweza kusababisha mali za Bakwata Baraza la Wadhamini litahakiki mali zote, kuziwekea wakfu ili kuzilinda, “Changamoto za kimfumo huwezi kuziondoa ila kwa majibu ya kimfumo. Kwa hiyo, changamoto za ubadhirifu na ufisadi uliokuwa unafanywa katika mali za wakfu za Waislamu tumeona jibu lake ni kuwa na kipengele cha kikatiba kinachozuia kuuzwa kwa mali za wakfu,” alisema.
Kuhusu mapato alisema ndani ya Bakwata mlikuwa na pakacha lililokuwa linasababisha kupotea kwa mapato na kwamba sasa kutakuwa na mfumo wa ukusanyaji kuanzia ngazi za chini hadi taifa.
“Ili kuutekeleza mfumo huu, Bakwata itaweka wahasibu katika mikoa yote na wilaya zote 196. Kutokana na hali ya Baraza ndio kwanza linajijenga, tunatoa wito kwa Waislamu wenye taaluma za uhasibu wajitokeze kuja kujitolea.”

No comments:

Post a Comment