Kwa kifupi mwajiri anafikiri namna bora zaidi ya kutumia uwezo na vipawa vyako kwa manufaa yake kubwa ikiwa ni kutengeneza faida huku wewe pengine lengo lako ni moja tu kupata ujira japo inaweza kuwa zaidi ya hapo.
Katika mahusiano haya mara nyingi ni vyema kupeana taarifa zitakazo tuwezesha kuimarisha mahusiano yetu katika ajira lakini pia kufanya maamuzi sahihi.
Kwa bahati mbaya mara nyingi mwajiri au bosi wako hawezi kukupa taarifa zote unazozihitaji kwa sababu mbali mbali ila moja kubwa ikiwa ni apate kukutumia vyema.
Kuna baadhi ya mambo napenda kukushirikisha ambayo pengine unayajua na unayaona ya kawaida lakini inawezekana hauyajui kabisa.
Lengo la kukushirikisha mambo haya si kwa lengo la kukufanya utofautiane na mwajiri wako lakini kwa lengo la kukufanya uelewe thamani yako lakini pia utambue kuwa kuna maisha nje ya ajira zetu lakini suala jingine la msingi ni uwe mnyenyekevu na kuishi vyema na watu wengine nje na ndani ya ajira yako Ukifa Mwajiri wako atatafuta mtu mwingine.
Inawezekana unapenda sana ajira yako na uko tayari kutumia muda wako mwingi hadi ule wa ziada ili kuhakikisha mambo yanaenda sawa ofisini kwako na taasisi inafikia malengo.
Hili si jambo baya ni jema na shauku ya kila mwajiri kuona wafanyakazi wote wanakuwa na mtazamo huu. Pamoja na hayo kumbuka kuwa kazi unayofanya ni sehemu fulani tu ya maisha na kuna maisha mengine zaidi ya ajira au kazi yako.
Jitahidi kazi isiwe sababu ya kukuletea maradhi au kukusababishia umauti.
Kwa sababu ukipoteza maisha pamoja na kwamba mwajiri wako atasema msibani ‘pengo lako halitazibika’
baada ya siku kadhaa atatangaza nafasi uliyoiacha kuliziba pengo na pengine atapatikana mtu bora zaidi yako.
Kuna mengi ya kujifunza hapa; kama hatuishi milele basi na ajira yenyewe siyo ya milele. Jifunze kuishi maisha ya kujipenda, tapata muda wa kuichunguza afya yako, jiepushe na mazingira hatarishi kwenye ajira yako na pia ishi na watu vizuri bila kujali nyadhfa wala elimu zao. Kwa kifupi ajira yako isiwe chanzo cha matatizo ya kiafya wala kijamii.
Mwajiri hawezi kukulipa zaidi ya kile unachozalisha
Lengo la mwajiri yoyote ni kuhakikisha anatumia ujuzi na maarifa yako katika kuiletea tija taasisi. Ujira unaopata ni sehemu ndogo ya kile kikubwa unachozalisha kama mtu mmoja au kwa ujumla na waajiriwa wengine. Wala sisisemi kwa kuajiriwa tunadhurumiwa, hapana, nachojaribu kukumbusha ni kuwa uwezo na ujuzi wako unathamani zaidi ya mshahara unaoupata na huu ni mfumo unaokubalika kwa sababu mwajiri naye analengo la kupata faida. Kama unahisi nakutania anza kutega kazini au fanya uzalishaji chini kiwango ulichowekewa na mwajiri wako. Utaachishwa kazi kwa kutokuwa mfanisi. Suala hili pia linatukumbusha kuwa tunauwezo wa kutumia uwezo na ujuzi wetu kuanzisha biashara au miradi binafsi na siyo tu kuacha vipawa, uwezo na ujuzi tulio nao kutumika na mwajiri pekee.
Mafanikio yako ni ya taasisi pia lakini makosa yako ni yako mwenyewe
Kuna vitu huendelea nyuma ya pazia ambavyo pengine hauvifahmu kwa sababu haujapata muda kusikia taarifa zinazozungumzwa juu yako. Ukiwekewa lengo na mwajiri na ukalifikia kwa namna moja ama nyigine umeisaidia kufikia mafanikio ya taasisi. Katika mazingira haya mkuu wako wa idara anaweza toa taarifa kwa wakuu wake kwamba idara yake inafanya vizuri sana kwa sababu tu ya jitihada zako. Katika mazingira hayo hayo endapo utafanya makossa waweza jikuta unasimama peke yako na lawama zikakuangukia ‘idara yetu haijafikia malengo kwa sababu John alisababisha hasara ya milioni 5’. Hapa mkuu wako anajitoa na kujiweka pembeni.
Hii inatupa somo kuwa kuna umuhimu wa kuhakikisha tunafanya shughuli zetu kwa umakini mkubwa na jitihada pia. Lakini tunajifunza kutofanya ofisi zetu kama ndiyo kila kitu kwa sababu kuna siku tutasimama wenyewe kuwajibika kwa kile ammbacho pengine tulikifanya kwa lengo zuri lakini mambo hayakwenda sawa.
Ukistafu Kazi Taasisi Haitakuwa na Muda na wewe
Kwa sababu taasisi nyingi zipo kibiashara kinachofanyika ni kuwatumia watu kama njia ya kufikia malengo ya kibiashara lakini pale wanapokuwa hawahitajiki tena wanakuwa mizigo na hasara kwa taasisi. Muda wako wa ajira utakapo koma uhusiano wako na mwajiri au taasisi nao unakoma pia. Kuna mengi ya kujifunza hapa pia. Moja, kuna ulazima wa kujipanga mapema kuyakabili maisha baada ya ajira lakini pili, kuishi na watu vizuri nje na ndani ya taasisi na kuhakikisha ajira yako haikupi kiburi cha kuwadharau na kuwanyanyasa wengine. Mtu unaye mtegemea atakuwa msada kwako kukukingia kifua utakapo anza kupata madhara ya matendo yako naye si wa kudumu hapo ni wa kuja na kuondoka-kuwa mpole.
Ni vyema kujifunza kutumia ajira hizi za muda kutengeneza heshima ya kudumu. Nyadhfa, vyeo na fursa mbali mbali katika ajira zetu zina ukomo hivyo si vyema vikawa vyanzo vya kujiharibia sifa njema. Mtu mmoja aliwahi kunambia ‘Fanya kazi vizuri, fuata taratibu, kuwa mfanisi lakini kumbuka ofisi hi siyo ya baba yako.
Mwisho, mzunguko wa maisha una sehemu nyingi sana; familia, imani, marafiki, ndugu, michezo, buradani na mambo kadha wa kadha. Kumbuka kuwa yote haya yana umuhimu wake na usisahau kuyatengea muda. Kazi na ajira ni muhimu sana lakini haiwezi kwenda peke yake-changa karata zako vizuri.
No comments:
Post a Comment