Anthony, mtoto wa miaka 10, mkazi wa Ngara alisimama kidete kumzuia baba yake Petro Magogwa asiuze nyumba yao, iliyokuwa mali pekee wanayoitegemea.
Katika habari hiyo, Anthony alimzuia baba yake asiuze nyumba na kutishia kumburuza polisi, akieleza kuwa anafanya hivyo ili familia yao, wakiwamo dada zake wasikose mahali pa kuishi.
Baada ya Mwananchi kuchapisha taarifa zinazoonyesha ujasiri wa mtoto huyo, wasamaria wema wamejitokeza kuisaidia familia hiyo na sasa watajengewa nyumba ya kisasa. Miongoni mwa waliojitokeza kumjengea nyumba ni mtangazaji wa Redio Clouds na mmiliki wa mitandao ya kijamii, Millard Ayo ambaye amejitolea kujenga nyumba nzima kwa gharama zake.
Pia, uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, umeahidi kuihamisha familia hiyo kutoka Kitongoji cha Mukitano, baada ya kubaini kuwa inaishi katika mazingira hatarishi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Aidan Bahama alisema Millard Ayo ameahidi kujenga nyumba hiyo na halmashauri itanunua kiwanja.
“Kiwanja kimepatikana kwa Sh4 milioni na tunataka kuhakikisha wanajengewa nyumba bora mzee huyu na watoto wake waishi kiafya na kiusalama,” alisema.
Mfadhili mwingine aliyejitokeza ni mmiliki wa Shule ya Amani Humwe, (Mwanga, Kilimanjaro), Isihaka Msuya ambaye ameahidi kumsomesha Anthony katika shule zake na kugharimia mahitaji yake yote.
Bahama alisema dada zake Anthony nao wanatafutiwa shule nyingine hivyo wanaojitokeza kusaidia familia hiyo wawasilishe michango yao kupitia akaunti ya Benki ya CRDB ya halmashauri hiyo au ofisi ya ustawi katika eneo hilo.
“Anthony atapelekwa shule wiki ijayo kuwahi masomo maana anaelekea sehemu ya ugenini hivyo anahitaji msaada zaidi wa kitaaluma kwa kupewa muda wa ziada” alisema.
Akizungumza kwa simu, Msuya alisema ameguswa na maisha ya mtoto huyo baada ya kusoma taarifa zake. Aliahidi pia kumtafutia mwalimu wa ziada kumfundisha ili aweze kwenda sambamba na wenzake.
“Nawahakikishia Watanzania na wenye kuguswa na maisha ya mtoto huyo kwamba atakuwa mazingira salama yenye kujali afya yake na kumsaidia aweze kutimiza ndoto za maisha yake,” alisema Msuya.
Baba mzazi wa Anthony, Petro Magogwa aliwashukuru wasamaria wema waliojitokeza kumsaidia na watoto wake na kueleza kuwa wakipata elimu itakuwa urithi wa maisha yao.
Mbali ya wahisani hao, Bahama alisema misaada mingine imeendelea kumiminika ndani na nje ya wilaya hiyo. Alisema wafanyakazi wa sekta mbalimbali wamechanga kiasi cha Sh 2.1 milioni, kati ya hizo, Sh 1 milioni ni ahadi.
Michango mingine ya Anthony imekuwa ikitolewa na wananchi kupitia namba ya simu inayoendeshwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), ambayo imeahidi kutangaza kiasi kilichopatikana kwa ajili ya mtoto huyo hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment