Kesi hizo namba nne na sita za mwaka huu, zilizofunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam dhidi ya AG zinahusu namna ya uendeshaji wa shughuli za siasa nchini, yakiwamo maandamano na wasimamizi wa uchaguzi.
Katika kesi namba nne wadai Francis Garatwa, Baraka Mwago na Allan Mwakatumbula wanaowakilishwa na Wakili Jebra Kambole, wanapinga vifungu namba 43, 44. 45 na 46 vya Sheria ya Jeshi la Polisi na kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa.
Katika kesi namba sita, mdai Bob Chacha Wangwe anayewakilishwa na Wakili Fatma Karume, anapinga wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Kesi hizo zilitajwa jana katika majopo mawili tofauti ya majaji, ambayo yote yanaongozwa na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali na katika kesi zote mdaiwa (AG) kupitia Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Alesia Mbuya ameieleza Mahakama kuwa wamewasilisha mapingamizi ya awali.
Wakili Mbuya ambaye alikuwa akisaidiana na mawakili wa Serikali wakuu, Abubakar Murisha na Aida Kisumo, aliomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya usikilizwaji wa mapingamizi hayo ya awali.
Jaji Wambali alikubaliana na maombi hayo na akaelekeza kuwa kama sheria na kanuni zinavyoelekeza, kesi hizo zitahamishwa kwa jaji mmoja kwa ajili ya kusikiliza na kutolea uamuzi mapingamizi hayo kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi za msingi (ikiwa mapingamizi hayo yatakataliwa).
Akitoa amri za Mahakama katika kesi namba nne, Jaji Wambali kwa niaba ya majaji wenzake, Rose Teemba na Rehema Sameji, aliamuru kesi hiyo itajwe Aprili 20, mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya usikilizwaji wa mapingamizi hayo.
Katika kesi namba sita, Jaji Wambali aliamuru kesi hiyo itajwe Aprili 17, mwaka huu kwa ajili ya kupanga tarehe ya usikilizwaji wa mapingamizi hayo kwa jaji atakayepangwa.
Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili Karume alitaja mapingamizi hayo yaliyowasilishwa na AG kuwa ni hati za viapo vinavyounga mkono kesi hizo zina upungufu wa kisheria, kesi hizo zimefunguliwa isivyo sahihi kisheria na pia hazina maana bali ni za kuudhi tu zenye kupoteza muda wa Mahakama.
No comments:
Post a Comment