Friday, April 6

Heche mbunge wa 16 kuwa nje kwa dhamana kortini


Kupandishwa kizimbani kwa mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kusomewa mashtaka matatu na kuachiwa kwa dhamana kumefanya idadi ya wabunge waliokumbana na hali kama hiyo kufikia 16.
Kesi zinazowakabili wabunge waliopo nje kwa dhamana ambazo wachambuzi wa siasa waliozungumza na Mwananchi wamesema hazileti picha nzuri katika siasa ya Tanzania, huenda zikaongezeka kutokana na jana mbunge mwingine, Ester Bulaya (Bunda Mjini) kuhojiwa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam na kuachiwa kwa dhamana.
Heche aliyekamatwa mahakamani hapo Jumanne iliyopita pamoja na wafuasi 23 wa chama hicho wakati wa kesi inayowakabili viongozi saba wa Chadema akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe, jana alifikishwa katika mahakama hiyo na kuunganishwa katika kesi ya viongozi hao na kusomewa mashtaka matatu ikiwamo kuchochea chuki.
Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai Heche na wenzake hao saba kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu maeneo ya viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 112 ya 2018 ambao wapo nje kwa dhamana ni Mbowe; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Wengine ni Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Heche alikana na Aprili 16 mwaka huu yeye na wenzake saba watasomewa maelezo ya awali mahakamani hapo.
Heche aliachiwa baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wenye barua za viongozi wa mtaa, vijiji au waajiri wao na nakala za vitambulisho.
Kama ilivyokuwa kwa viongozi saba wa chama hicho, wadhamini wa Heche nao walisaini ‘bondi’ ya Sh20 milioni huku mbunge huyo akitakiwa kuripoti polisi kila Alhamisi.
Mbali na wabunge Heche, Mbowe, Mchungaji Msigwa, Mdee, Matiko na Mnyika, wabunge wengine wenye kesi na wako nje kwa dhamana ni Peter Lijualikali (Kilombero), Susan Kiwanga (Mlimba), Saed Kubenea (Ubungo), Godbless Lema (Arusha Mjini).
Wengine ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Cecil Mwambe (Ndanda), Kunti Yusuph na Zubeda Sukuru (wote viti maalumu) na Frank Mwakajoka (Tunduma) na Paschal Haonga (Mbozi).
Hata hivyo, jeshi la polisi limekuwa likisema mara kwa mara kuwa linapowakamata watu na kuwafikisha mahakamani huwa haliangalii kama ni wanasiasa au watu maarufu ila huangalia wahalifu.
Wachambuzi wanena
Mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa waziri katika Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Njelu Kasaka alisema, “hili ni jambo jipya ambalo huko nyuma halikuwepo. Taifa linapaswa kujiuliza kwa nini wabunge wengi wana kesi.”
Kasaka aliyekuwa miongoni mwa wabunge waliounda kundi la G55 lililoibuka na hoja ya Muungano wa Serikali tatu mwaka 1993 aliongeza kuwa, “nafikiri tufike wakati kama Taifa tuone jinsi ya kuyamaliza bila kufikishana mahakamani.”
Alitolea mfano mataifa ya Korea Kusini na Marekani ambayo yalikuwa yakitishiana kwa makombora.
“Waliona wataangamiza wengi, wamekaa chini na kuyamaliza. Jambo kama hili linaweza kufanywa na viongozi tulionao, wana uwezo wa kuyamaliza na tukawa na maelewano mazuri kama huko nyuma,” alisisitiza.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alipingana na Kisaka na kubainisha kuwa huenda ukawa mkakati wa wapinzani kuendelea kuandikwa na vyombo vya habari na kudai hauna afya kwa wapiga kura waliowachagua.
“Wananchi wamekuchagua ukawawakilishe lakini wewe unashinda mahakamani badala ya kushinda nao kutatua kero zinazowakabili unabaki kupambana na kesi. Hii inawajengea kutokuaminika tena,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba aliunga mkono hoja ya Kasaka na kuongeza kuwa wapinzani hawapaswi kuonekana kama wakosaji bali wachukuliwe ni sehemu ya jamii yenye manufaa makubwa. “Hiki kinachotokea sasa kama kingetokea mwaka 1995 au 1996 wakati upinzani unaanza tungeelewa, lakini si sasa ambapo tumeshuhudia upinzani ukiibua hoja zenye manufaa kama Escrow au Epa. Bila upinzani madhubuti hatuwezi kuwa na Taifa imara,” alisema Dk Bisimba.
“Kama wanataka kuua upinzani na kubaki chama kimoja watambue wanazalisha upinzani ndani ya chama hicho kimoja kwani hata G55 ilianzishwa ndani ya chama kimoja, kwa hiyo upinzani waachwe wawe huru na waikosoe Serikali ndio moja ya wajibu wao.”

No comments:

Post a Comment