Friday, April 6

Rufaa ya Wambura TFF yatupwa


Mwenyekiti wa kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili  Ebenezer Stafford Mshana ametupilia mbali rufaa ya aliyekuwa makamu wa rais wa TFF, Michael Wambura.
Wakili Mshana amesoma hukumu ya rufaa hiyo leo Aprili 6 makao makuu ya TFF, Karume jijini Dar es Salaam na kutangaza kutupilia mbali rufaa hiyo.
Wambura alikata rufaa kwenye kamati hiyo kupinga uamuzi wa kamati ya maadili kumfungia maisha kujihusisha na masuala ya soka kwa makosa matatu.
Makosa hayo ni kupokea/kuchukuwa fedha zaTFF za malipo ambayo hayakuwa halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013
 Jingine ni kughushi barua ya kueleza alipwe malipo ya Kampuni ya Jekc System Limited huku akijua malipo hayo sio halali ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(7) cha Kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013
 Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa 2015.
Hata hivyo, Wakili Ebenezer alisema Wambura anaweza kupeleka malalamiko yake kwenye mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa michezo (CAS).
"Hapa nchini baada ya hukumu hii, Wambura hawezi kupinga mahali pengine popote labda aende CAS kwa kuwa kamati hii ndiyo yenye uamuzi wa mwisho," alisema.
Wambura alishtakiwa na Sekretarieti ya TFF baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura kuonekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili iliyotangaza kumfungia maisha katikati ya Machi.
Kigogo huyo wa mpira alinga uamuzi wa kamati ya maadili na kukuta rufaa, huku rais wa TFF, Wallace Karia akimtaja Athuman Nyamlani kukaimu nafasi ya Wambura TFF siku kadhaa zilizopita.
Karia alikaririwa na Mwananchi hivi karibuni akibainisha kuwa uteuzi wa Nyamlani umefanyika kwa matakwa ya katiba ya Shirikisho lakini pia akasisitiza ni haki ya rufaa ya Wambura kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment