Saturday, April 7

Tanzania yaanza vibaya Madola Australia


Tanzania imeanza vibaya Michezo ya Madola mjini Gold Coast, Australia baada ya muogeleaji Hilal Hilal kushindwa kuingia fainali mita 50 katika staili ya ‘butterfly’.
Pamoja na kumaliza katika nafasi ya tatu kwa kupata muda wa 26.32, Hilal amekuwa wa 35 kati ya waogeleaji 56 walioshindania nafasi 16 bora za kufuzu fainali. Hata hivyo, muogeleaji huyo ameimarisha muda wake 0.8 tofauti na muda wake wa awali 26.40.
Muogeleaji wa Afrika Kusini, Chad Le Clos amekuwa wa kwanza katika orodha hiyo kwa kutumia muda 23.53 na kufautiwa na Dylan Carter wa Trinidad and Tobago aliyetumia muda 23.62. Pia nafasi ya tatu ilichukuliwa na muogeleaji wa Afrika Kusini, Ryan Coetzee aliyepata muda 23.94.
Katika hatua ya kufuzu, Mkenya, Steven Maina aliibuka katika nafasi ya kwanza baada ya kupata muda 26.02 na kufuatiwa na Erico Cuna wa Msumbiji aliyepata muda 26.11.
Matokeo haya ni pigo kwa Tanzania ambayo tangu mwaka 2006, haikuwahi kushinda medali katika michezo hiyo. Hata hivyo, Hilal ana nafasi ya kurekebisha makosa kwa kuwa atawania tena medali katika mita 100 kwenye ‘freestyle’.
“Hilal amejitahidi sana pamoja na matokeo hayo, hata hivyo, muda wake umeonyesha kuna medali katika siku za usoni katika mchezo wa kuogelea, bado ana nafasi ya kurekebisha makosa katika shindano linalofuata la ‘freestyle’ mita 100,” alisema Yusuph Singo ambaye ni mkuu wa msafara wa timu ya Tanzania.
Wakati huo huo, mabondia wawili akiwemo mkongwe Selemani Kidunda na Haruna Mhando leo wanawania nafasi ya kushinda medali katika ukumbi wa Oxernford Studio.
Wakati Mhando atapambana na bondia wa Kenya, Edwin Owuor katika mzunguko wa 32, Kidunda atapambana na bondia kutoka China, Naman Tanwar katika uzito wa kati wa kilo 75 kuwania nafasi ya kufuzu robo fainali.

No comments:

Post a Comment