Saturday, April 7

Gambo: Nitakuwa wa mwisho kufa katika vita vya uchumi


Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amemwambia Rais John Magufuli kuwa atakuwa naye hadi atakapokufa, akimsaidia katika vita ya kiuchumi.
Gambo ameyasema hayo leo Aprili 7 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha wakati Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuzindua kituo cha polisi na nyumba 31 za polisi.
“Nikuhakikishie kuwa nitakuwa mtu wa mwisho kufa hadi vita uliyoanzisha inafikia mwisho,”amesema.
Gambo amesema kuna watu ambao wanakwamisha kwa makusudi juhudi za Rais na wanataka viongozi wengine wasimpe ushirikiano na hivyo akasema yeye atakuwa pamoja na Rais Magufuli mpaka mwisho.
“Nia yao ni kuona tunakuacha peke yako, lakini hatutafanya hivyo, tutakuwa na wewe katika vita hii mpaka mwisho,” amesema.
Pia, amesema wapinzani wamekuwa wakilalamikia mambo mengi ikiwamo suala la ndege, lakini ndege imekuja na bado wanasema.
“Umeleta ndege sita, sasa wanalalamika mbona umenunua hii na kuacha kile. Hawa ni popo siyo ndege wala wanyama hivyo usihangaike nao,” amesema na kuongeza:
“Wapinzani wangependa wote tukate tamaa ili ubaki peke yako, mimi kama msaidizi wako nakuhakikishia nitakuwa wa mwisho kufa katika vita hii.”

No comments:

Post a Comment