Saturday, March 3

Wizara kushauri uundwaji wa jeshi jipya mahsusi kwa misitu na wanyamapori


Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangalla amesema wizara ipo kwenye mchakato wa kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Jeshi jipya litakalokuwa maalumu kwa usimamizi wa wanyamapori na rasilimali za misitu nchini ili kuboresha utendaji kazi katika sekta hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti na kusimamia sekta ya maliasili kutokana na kuingiliwa na majangili wanaosababisha rasilimali hiyo kuteketea. 
"Vikosi vya majeshi vilileta ushauri huo na sasa wizara tumeona jambo hilo lina tija kweli, hivyo tupo kwenye mchakato huo na tumefikia hatua nzuri tukikamilisha tunampelekea Rais kwa kumshauri aanzishe jeshi jipya kwa ajili wanyamapori na misitu, tunaamini jambo hili litazaa matunda,” amesema.
Amefafanua kuwa jeshi litakaloundwa litakuwa chini ya Rais mwenyewe na litasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kujenga nidhamu kwa watumishi.
Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Misitu Tanzania,(TFS) Professa Dos Santos Silayo amesema kwa sasa wameimarisha utendaji wa wakala huo tofauti na ilivyokuwa awali wa kusimamia mapato  tu.
Amesema hatua ya kubadili wakala huo na kuwa mamlaka kamili ya misitu itaongeza ufanisi na utendaji kazi katika sekta hiyo. 
"Mbali na kuweka mifumo mizuri ya udhibiti lakini tumeanza ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi karibu na misitu ili kuweka ulinzi wa rasirimali hizo.”

No comments:

Post a Comment