Wednesday, March 7

Waziri ataka wachimbaji wadogo 400 kuondoka eneo la mwekezaji


Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wachimbaji wadogo zaidi ya 400 waliovamia eneo la uchimbaji katika Kijiji cha Bululu, Kata ya Nyamtukuza, Wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita kuondoka katika eneo hilo kwa kuwa lina leseni ya mwekezaji.
Eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 13.6 lina leseni 24 za uchimbaji chini ya kampuni ya madini ya Nyanzaga ambayo ilikata leseni ya utafiti wa madini namba PL 9662 ya mwaka 2014 ambayo inaisha muda wake Machi 30.
Akizungumza jana Machi 6, 2018 na wachimbaji hao,  Biteko amesema nia ya Serikali ni kutoa maeneo ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika na rasilimali hiyo, lakini akawataka kuheshimu sheria hadi pale muda wa mwekezaji utakapomalizika.
"Ni jambo la kusikitisha wilaya nzima kukosa eneo la
wachimbaji wadogo, taarifa niliyopata ni kwamba maeneo yote yana leseni za wawekezaji na hawajazifanyia kazi, niwaombe mtulie msiharibu mambo huyu leseni yake ndio inafika mwisho mkichimba mnampa nafasi ya kushtaki na hamtapata, vuteni subira zimebaki siku chache,” amesema Biteko.
Amesema  kwa sasa leseni ambazo zimeshikiliwa na mwekezaji na hajaendeleza eneo zikiisha muda wake wizara inazigawa kwa wachimbaji wadogo na kuwataka wajiunge kwenye vikundi kwa kuwa leseni hazitolewi kwa mtu mmoja mmoja.
Awali, Mbunge wa Nyang’wale,  Hussein Kasu amesema  wananchi wamechoka kukimbizwa kwenye maeneo kila wanapovumbua eneo lenye dhahabu na kusema sasa wamefika mwisho na hawapo tayari kuendelea kuonewa.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mkoani Geita, Christopher Kadeo amesema changamoto kubwa katika sekta ya madini ni maeneo mengi kuwa na leseni kubwa za utafiti ambazo hazifanyiwi kazi huku wachimbaji wadogo wakiwa hawana maeneo.

No comments:

Post a Comment