Wednesday, March 7

Muswada tata wa mabadiliko ya Katiba wazua wasiwasi Kenya


Miezi michache iliyopita nilisema katika makala yangu moja kwamba pilikapilika za siasa za mwaka 2022 nchini Kenya zingeanza punde tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuanza utawala wake wa muhula wa pili na wa mwisho. Utabiri huo ulitimia hata kabla sijafumba wala kufumbua jicho.
Siasa za kumalizana au kujengana kuelekea mwaka huo sasa zimejaa tele nchini. Kila mwanasiasa anajaribu kila awezalo kuchora ramani yake itakayompa nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi ya mwaka 2022.
Kiti cha urais ndicho kinaleta utata na migawanyiko ambayo inaenda kasi kuliko vile tunavyoweza kuichambua au kubashiri jinsi itakavyopinda na kunyooka katika siku zinazokuja.
Mambo mazito
Kimsingi, wale wanaokosoa Serikali wamejikuta mahali pabaya huku wakipoteza viti vyao vya ubunge katika mahakama mbalimbali.
Na mambo bado. Ghafla bin vuu, mbunge wa chama cha Kanu, William Kamket awasilisha muswada katika Bunge la Kitaifa akitaka Katiba ibadilishwe kutoa nafasi ya wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka tele na kiongozi wa shughuli za Serikali.
Isitoshe, muswada huo unatafuta kupunguzwa kwa nguvu za Rais. Ikiwa muswada huo utapitishwa na Bunge, Rais hatakuwa na mamlaka kama ilivyo sasa.
Licha ya hayo, muswada huo ukipitishwa, Rais atakuwa na muhula mmoja tu wa miaka saba wa kutawala kinyume na sasa ambapo rais anaweza kuwania kiti hicho mara mbili mfululizo; kila muhula una miaka mitano.
Mswada wa Kamket una nafasi mbili za makamu wa rais; kwa hivyo ukipita, kutakuwa na makamu wa rais wawili.
Wachambuzi wa siasa wanasema ingawa muswada huu uliletwa na Kamket kama muswada wa binafsi, kuna watu wanaoufadhili kwa ajili ya kunufaisha wanasiasa fulani mnamo 2022 wakati Kenya itakuwa inawachagua wanasiasa wao akiwemo rais wa kumrithi Uhuru.
Rais Uhuru amejitenga na muswada huo akisema jukumu lake sasa ni kuzingatia miradi ya maendeleo. Aliongeza kwamba yeye hatajiingiza kwenye siasa baada ya 2022.
Ili kuelewa kwa nini muswada huu unakuja wakati huu, ni muhimu kuelewa nguvu zinazokinzana katika jukwaa la kisiasa zikilenga uchaguzi wa 2022. Rais Uhuru amesisitiza kwamba atamuunga mkono makamu wake, William Ruto anayepania kumrithi.
Lakini si wote wanaoimba pambio hili. Baadhi ya wanasiasa wa chama cha Jubilee wanaichimbia kaburi fursa ya Ruto; wanasema hawaungi mkono ndoto zake za urais. Wanasiasa hao wanaegemea upande wa Seneta wa Baringo, Gideon Moi.
Gideon ni mwanaye Rais mstaafu, Daniel arap Moi. Uhusiano wake na Ruto kisiasa ni mbaya mno na wanachosubiri wanasiasa hao ni kutoana kijasho 2022.
Gideon ni mwenyekiti wa chama cha Kanu ambacho alikirithi kutoka kwa babake alipostaafu 2002. Wadadisi wa siasa wanasema Seneta huyo ndiye amemtuma Kamket kuwasilisha mswada huo bungeni ili uhujumu ndoto za Ruto.
Kiongozi wa walio wengi bungeni, Adan Duale amefuata nyayo za Rais Uhuru kwa kusema kamwe hatakubali kupitishwa kwa muswada huo bungeni.
Kanu iliunga mkono chama cha Jubilee katika uchaguzi wa mwaka jana ikitarajia kufaidika kutokana na nyadhifa mbalimbali serikalini, lakini waliambulia patupu wakati Rais na Makamu wake walipounda Serikali.
Hatua hii huenda iliwatuma wana Kanu kufikiria upya uhusiano wao na Jubilee na hatma ya baadaye ya kiongozi wao. Kanu iko mbioni kutafuta njia na marafiki wapya katika safari hii ndefu iliyojaa hatari ya kuelekea 2022.
Lakini muswada huo ukipitishwa, unaweza kupokea uungwaji mkono kutoka kwa mirengo mbalimbali ikiwemo ya upinzani.
Kauli ya OdInga
Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga amepinga vikali muswada huo akisema hautapita. Kuna dalili Raila atawania tena urais 2022 baada ya uhusiano wake na viongozi wenza wa upinzani kukwama kwenye bahari ya Muungano wa Nasa. Muungano huu unayumbayumba huku Raila akilalama kwamba haitakuwa muda mrefu kabla ya viongozi wenza wake kumsaliti kama vile Yesu Kristo alivyosalitiwa na Yuda.
Ikiwa anawania urais, Raila hatataka kuwa Rais asiye na mamlaka ya kutosha.
Ruto naye amepuuzia mbali muswada huo akisema wakati wa kufanya siasa umeisha na wale wanaotaka kupoteza muda kwa siasa zisizo na maana wanafaa kusubiri hadi 2022.
Jamii ya Wakikuyu ambayo ni kabila la Rais Uhuru imegawanyika katikati kuhusu endapo watampigia kura Ruto 2022 kama shukrani kwa kumuunga mkono mara mbili kijana wao Uhuru (2013 na 2017).
Lakini familia ya Mzee Moi pamoja na wafuasi wa Kanu hawataki kusikia wala kusimuliwa juu ya ndoto za Ruto kumrithi Uhuru.
Miezi miwili iliyopita, Gideon na nduguye Raymond walihutubia wanahabari wakisema Wakikuyu hawana deni lolote la kisiasa kwa mtu yeyote kumaanisha kwamba si lazima kabila hilo limpigie Ruto kura 2022.
Lakini kulingana na makubaliano kati ya Uhuru na Ruto, Wakikuyu hawana budi kumpigia Makamu wa Rais kura awe rais wa tano wa Kenya.
Muswada huu unaweza kusambaratisha ndoto hizo lakini ikiwa utapita. Na je, utapita vipi huku Jubilee ikiwa na wabunge wengi zaidi kuliko vyama vingine?
Lakini ukipitishwa kwa uungwaji mkono wa Jubilee na Baraka za Rais Uhuru, Ruto anaweza kufaidika kwa sababu atakuwa na nyadhifa nyingi za kuwagawia wale watakaomuunga mkono kuliko kujistarehesha bila hakikisho la kuungwa mkono na Wakikuyu pale Uhuru atakapostaafu.
Ruto anaweza kumwamini Rais Uhuru anaposema hatamuacha 2022 lakini Uhuru hana uwezo wa kuwalazimisha Wakikuyu wote popote walipo kumpigia kura Ruto.
Katika miaka iliyopita, jamii ya Wakikuyu imeenda kinyume na ahadi zilizotolewa na viongozi wao kwa wale waliowaunga mikono kunyakua urais.
Mbali na hayo, Kanu imesema wanaunga mkono Muswada wa Kamket kwa kuwa unalenga kuleta mazuri katika uongozi. Ni mapema kwa Jubilee kuonyesha ishara zozote za kupigia debe muswada huo lakini kuna uwezekano wa mtazamo huu kubadilika.
Katika Kanda ya Afrika Mashariki, si jambo geni kwa wanasiasa kubadilisha Katiba ili kuwapa viongozi fulani nafasi ya kuongoza au kuendelea kuongoza kwa muda mrefu.
Mfano mzuri ni Rwanda ambapo utawala wa urais wa miaka saba umepangwa na kutekelezwa. Uganda pia ina mpango kama huu. Huenda watu fulani katika Jubilee wanataka Rais Uhuru kuendelea uongozini kwa kuwania kiti cha waziri mkuu.
Rais Uhuru ataendelea kuwa mwenyekiti wa chama cha Jubilee baada ya kustaafu lakini pia kuna uwezekano kuwa anaweza kuendelea kuongoza ikiwa muswada huu utapitishwa kwa kuungwa mkono na Jubilee.
Kwa sasa, wabunge na viongozi wa Jubilee hawataki kuonekana kuunga mkono mswada huu kwa sababu uongozi wa chama chao haujafikia uamuzi mahsusi.
Lakini kwa sababu ya siasa zetu ambazo jamii nyingine zinafungiwa nje ya uongozi, muswada huu unaweza kuwa tiba kamili ya kuwaleta uongozini viongozi wa makabila mengine wanaohisi wamefungiwa nje ya uongozi muda mrefu.
Kamket anateta kuwa, muswada wake haulengi kukatisha ndoto za wanasiasa fulani bali unapania kuleta uwiano nchini. Pia anasema wabunge wengi wa Jubilee wanaufurahia na wanasubiri kwa hamu kuupitisha.

No comments:

Post a Comment