Bila kumwogopa Mungu, hatuwezi kupiga hatua kama taifa. Leo hii kilio kikubwa ni Katiba Mpya. Kila mtu anayetaka kujenga hoja ya kisiasa inayoendana na wakati wa sasa, ni lazima ataje katiba.
Ingawa kuna ukweli usiopingika kwamba kuna watu katika taifa letu hawataki kusikia neno Katiba, na hasa kutaja Katiba Mpya; bado asilimia kubwa wanaililia. Hata hivyo, hata tukiwa na katiba nzuri kiasi cha kuihamisha milima, bila kumwogopa Mungu, hatuwezi kufika popote.
Siasa zetu ziwe ni za kumwogopa Mungu. Tuvijenge vyama vyetu vya siasa kwa msingi wa kumwongopa Mungu. Tusiwe na lengo na kubomoa vyama vingine, tuheshimu uhuru wa kila Mtanzania. Ukweli ni kwamba tukimtanguliza Mungu, hatuwezi kujenga uhasama wa kisiasa, bali kila chama kitakuwa kikikamilisha chama kingine.
Usiwe ushindani wa vyama vya siasa, bali ushindani wa hoja na sera, usiwe ushindani wa ubora wa vyama vya siasa bali utekelezwaji wa sera, ubora wa kuheshimu haki za binadamu na kuutukuza na kuulinda uhai.
Mungu, anatuumba ili tumpende na kupendana sisi kwa sisi. Tukimwogopa Mungu, tutajenga ufalme wake hapa duniani. Siasa zetu zijengwe juu ya msingi imara wa kumwogopa, kumpenda na kumtumikia yeye peke yake.
Kuna kilio kikubwa cha kubinywa kwa demokrasia, chama kimoja kuwa na nguvu na upendeleo kuliko vingine. Kutokuwa na Tume huru ya uchaguzi; madai ya aliyeshindwa kutangazwa mshindi na aliyeshinda kutangazwa ameshindwa na Serikali kukibeba chama kimoja na vyombo vyote vya serikali kukitumikia.
Hiki ni kilio kinachosikika mipaka yote ya nchi yetu. Hata kama kilio hiki kingekoma leo, ukawepo usawa wa vyama vyote na demokrasia ikatawala, tukawa na Tume huru ya uchaguzi, bila ya kumwogopa Mungu si kitu si lolote.
Tunaambiwa kwamba kumwongopa Mungu ndiyo mwanzo wa maarifa na mafanikio. Wale wote waliotembea njia hii, wamefanikiwa. Ingawa taifa letu halina dini, watu wake wote wanamwamini Mungu. Tuna dini nyingi katika taifa letu; dini za kigeni na zile za jadi.
Dini zote zinahimiza kumwogopa Mungu, ili maisha yetu hapa duniani yawe ni ya kumtukuza yeye na kuwapenda na kuwajali ndugu zetu. Amani na utulivu katika mataifa ya dunia hii ni matokeo ya kumwogopa Mungu. Wale wanaopuuza ukweli huu, wanashuhudia vita na maangamizi makubwa.
Tumwogope Mungu, kwa matendo yetu mabaya, Tuongope kuwatendea ndugu zetu yale tusiyopenda kutendewa na sisi. Tumwogope tunapopokea sadaka na zaka nzito kutoka mikononi mwa wanasiasa, bila kuuliza wala kuhoji, tumwogope tunapowakumbatia wanasiasa wenye sifa za ufisadi na kuwaalika kuendesha harambee za kujenga misikiti na makanisa.
Tumwogope Mungu, tunaposamehewa kutoa ushuru na badala ya kuwahudumia wanyonge na maskini, tunajitenga na jamii na kuishi maisha kifahari. Tumwogope Mungu, tunapokula na kusaza, wakati wengine wanakufa kwa njaa.
Tumwogope Mungu, tunapoziingilia familia na kuzisambaratisha. Tumwogope Mungu, tunaposema uongo na kuwasingizia watu. Tumwogope pale tunaposhughulikia afya zetu kwenye hospitali nzuri na kuwaacha wanyonge kufa kwa magonjwa yanayotibika. Orodha ni ndefu. Ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya.
Kwa viongozi wetu wa dini za Kikristu, ujumbe huu unaweza kuwasaidia kutafakari zaidi:
“……. Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa shetani na malaika wake. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu hamkunipa maji; nilikuwa mgeni hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama…… Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi” ( Matayo 25: 41- 46).
Yesu, aliongelea mambo yanayotendeka kila siku katika jamii, mambo ambayo yanawatenga watu na Mungu wao. Hivyo orodha hii inaweza kurefushwa, “Mlinibagua kufuatana na rangi yangu ya mwili, kabila langu na dini yangu, chama changu, mlininyanyasa, hamkunisikiliza, hamkunionea huruma nilipolala mitaani, hamkunipatia ushauri mzuri mme wangu alipoanza kutembea nje ya ndoa na kuambukizwa na virusi vya Ukimwi, mlinibagua, mlinibaka, kuninyanyasa kijinsia... ”.
Orodha ni ndefu. Hoja ni kwamba ni lazima kumwogopa Mungu, kwa matendo yetu yote mabaya. Tumwogope na kumtanguliza kwa kila kitu, lakini tunatenda kinyume. Ni dhambi kubwa kujitangaza kuwa mikononi mwa Mungu, lakini huku unatenda kinyume, huko si kumwogopa Mungu.
Yule anayewanyanyasa wanawake na kuwanyima nafasi ya uongozi katika na nafasi ya kufanya maamuzi muhimu katika jamii kama vile ndoa na familia, kuzaa watoto wengi au kuzaa kwa mpango, kutoa mimba au kulinda uhai kwa kupoteza uhai (mfano mwanamke mwenye matatizo kwenye kizazi, ambaye kama angetoa mimba, angeponyesha maisha yake), kuhusu malezi nk, ni lazima amwogope Mungu, maana kuwabagua na kuwanyanyasa wanawake ni Kumbagua Mungu mwenyewe.
Tunafundishwa kwamba sote tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, na kwamba binadamu wote ni sawa. Bahati nzuri Katiba yetu inakubaliana na kitu hiki na ile Katiba Mpya tunayoililia imenyoosha vizuri zaidi.
Yule anayewabagua watu wa dini nyingine, ni lazima amwogope Mungu, maana sisi sote ni watoto wa Mungu. Tunaambiwa Mungu, alituumba kwa mfano wake, hivyo hatuna ruhusa ya kubaguana. Tukitaka kubaguana, tukumbuke kwamba ni lazima kumwogopa Mungu. Huwezi kumwogopa Mungu, huku unawabagua watu kwa sura zao, rangi zao, kabila zao, vyama vyao au dini zao.
Ukweli unaotuzunguka sasa hivi ni kwamba Waislamu wanajiona wana haki zaidi ya wengine, Wakristo pia wanajiona wana haki zaidi ya wengine. Wakristu wanagawanyika katika madhehebu ambayo kila dhehebu linajiona kuwa na haki zaidi ya mengine; Waislamu vilevile. Dini zinakuwa kikwazo cha ushirikiano, udugu kama vile ndoa nk, wakati mwingine hata viongozi wa Serikali wanachaguliwa si kwa sifa bali kwa kufuata dini zao.
Yule asiyependa majadiliano, ushauri, ushirikishwaji, ni lazima amwogope Mungu, maana Wakristo wanamwamini anayesikiliza, mwenye huruma , upendo na wema.
Yule asiyekuwa upande wa wanyonge na wanaoonewa, ni lazima amwogope Mungu, maana mbali na hukumu inayotajwa na Matayo katika sura ya 25, mstari wa 31 na kuendelea, Yesu, alisisitiza sana kuwajali wanyonge, wanaoonewa na wafungwa:
“Roho wa Bwana yu pamoja nami, kwani ameniteua rasmi niwaletee maskini habari Njema. Amenituma niwatangazie wafungwa kwamba watapata uhuru, vipofu watapata kuona tena; amenituma niwakomboe wanaoonewa, na niutangaze mwaka ambao Mungu atawakomboa watu wake” ( Luka 4:18-19).
Habari njema inakuja kwa maskini, wafungwa na wanaoonewa, si kwa matajiri na wenye madaraka. Ili ujumbe huu uwe na maana, Yesu mwenyewe alijitokeza miongoni mwa maskini na wanaoonewa. Alizaliwa katika umaskini na kukulia katika umaskini. Enzi zake kulikuwa na matajiri wenye majumba ya kifahari, lakini hakuyachagua. Aliishi na maskini. Mitume wake wote walikuwa ni watu maskini. Aliwaponya wagonjwa, waliwafufua wafu na kuwapatia uzima mpya, uzima tele. Maana yake uhai tele ndiyo kusema wito wetu ni wa uhai tele, kuulinda na kuutetea uhai. Wenye njaa aliwashibisha chakula cha mwili na roho, wenye kiu aliwapatia maji ya uzima. Alifanya miujiza mingi bila kudai ujira.
Hivyo yule anayefanya kazi na kudai ujira, ni lazima amwogope Mungu, maana tumepewa bure ni lazima kutoa bure. Kwenda kinyume na hayo ni maasi. Ukitaka ujira ni lazima umwogope Mungu. Ni lazima kumtanguliza Mungu, maana tumepewa bure na tutoe bure.
Ili ujumbe wa viongozi wetu wa dini uwe na maana yoyote ile ni lazima wajiulize wamesimama upande gani? Kuna matajiri na maskini, kuna majumba ya kifahari na kuna vibanda. Viongozi wetu wa dini wanaishi kwenye majumba ya kifahari au wanaishi kwenye vibanda? Wanapanda daladala au magari ya kifahari?
Je, wako upande wa maskini na wanaoonewa au upande wa matajiri na wenye madaraka. Je, wanaponya wagonjwa? Wenye njaa wanawapatia chakula? Wenye kiu wanawapatia maji ya kunywa? Je wanafanya miujiza bila ya kudai ujira?
Viongozi wetu wa dini wanapotukumbusha kumwogopa Mungu, ni bora wao wakatafakari je, wao wanamwogopa Mungu? Je, wao wanashiriki kiasi gani kuchangia hali hii ya watu kuishi bila kumwogopa Mungu. Kwanini watu waamue kuuza haki yao ya kupiga kura? Kwanini watu waamue kumchagua kiongozi si kufuata sifa zake bali wafuate kabila, dini, pesa, pilau na kanga wanazozipata wakati wa kampeni? Je, viongozi wetu wa dini wanachangia kiasi gani katika kuujenga uchumi wetu?
Kama bado kuna dalili za watu kufanya mambo bila kumwogopa Mungu, katika jamii yetu, basi viongozi wetu wa dini hawajafanya kazi yao vizuri. Mafundisho yao yatakuwa yanapeperushwa na upepo, hayajikiti katika jamii. Kutukumbusha ni jambo zuri, lakini pia kutengeneza mifumo ya kubadilisha hali hii mbaya ni jambo muhimu zaidi. Na mifumo hii itafanikiwa tu pale tutakapoanza kumwogopa Mungu.
Mungu, ametuumba ili tusaidiane na kukumbushana wajibu zetu. Mtu, akisimama peke yake anaanguka haraka. Bahati mbaya hatuna mfumo mzuri wa kukutana na kusaidiana. Watu wanaokutana kanisani au msikitini ni wengi kiasi ni vigumu mtu kumkaribia jirani yake na kumsaidia.
Tungekuwa na mpango wa familia chache kukutana, kusali pamoja, kujadiliana na kusaidiana kimawazo, ki- hali na mali, ungekuwa msaada mkubwa. Haya ndio viongozi wetu wa dini wangekuwa wakiyafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment