Wednesday, March 7

Mfumo wa kodi wa Jamhuri ya Muungano utazamwe upya


Akina mama wa ukanda wa pwani, bara na visiwani, wanao wimbo unaosikika sana wakati wa harusi.
Kila ukiimbwa wengi hushangilia ijapokuwa ujumbe wake ni wa kusikitisha.
Katika wimbo huu utamsikia mwana mama mmoja analalama kwa kusema “Mama naumia”. Kauli hiyo hufuatiwa kwa wenzake kuitikia
“Pole mwanangu” na wengine hubandika vibwagizo, “Ndio ukubwa au furaha hutanguliwa na karaha”
Kwa mara nyingine niliukumbuka wimbo huu niliousikia tangu mdogo na naendelea kuusikia kila wanapokusanyika akina mama kushangilia kile
wanachokiita bibi kapata bwana, yaani harusi. Kuna kilio kama hiki, lakini ninachoweza kusema ni cha “baba naumia” kinasikika sana siku hizi katika jamii ya Watanzania na hasa wa Visiwani. Anayelalama anaambiwa “Pole raia mwema”.
Kinachowaliza ni mfumo wetu wa kodi ambao unalalamikiwa na kuelezwa kwamba unambinya raia kushoto, kulia na pembeni.
Ukitaka kuelewa kwa kiasi gani hali ni mbaya tumia muda mfupi katika bandari ya Dar es Salaam inapofika boti kutoka Zanzibar.
Hapo mabegi hupekuliwa kama vile paka anafukua ardhi apate kujisaidia. Watu wanatozwa kodi hata wakibeba birika lililotumika la kuchemshia maji ya moto.
Wanaochukua mitumba ya runinga, hata uliotumika kwa muda mrefu, iwe kama zawadi au mtu anahama kikazi, utaona anapigwa bao la kutakiwa alipe
kodi ya shilingi laki mbili au tatu.
Watu hutozwa kodi hata kwa kitanda kilichotumika na wakati mwingine hata godoro na mito nayo hudaiwa kodi.
Ukitaka kujua sheria au mwongozo unaoainisha hayo makadirio, jawabu unalopata ni kama vile umebeba mali ya wizi licha ya kuwa na stakabadhi za kununulia ulichochua.
Siku moja niliamua kuacha pasi niliyotumia kwa miaka sita niliyokwenda nayo Dar es Salaam kumpa binti yangu ambaye pasi yake iliharibika na kuniomba kwa vile nilikuwa na ya ziada nimpelekee.
Tulibishana na huyo mtoza kodi, kijana ambaye sikujua kama ni askari polisi, ofisa wa forodha au Usalama wa Taifa.
Sikumjua kwa vile hakuwa na sare iliyomtambulisha ni mfanyakazi wa kitengo gani.
Hatimaye nilimtaka aichukue yeye kama zawadi ya kuimarisha muungano wetu kwa kuwa sikuona uhalali wa kuilipia kodi ya Sh15,000.
Nilipoiacha, alinifuata kutaka niilipie kodi na niichukue. Nilimwambia sikuwa na kawaida ya kuiba au kukubali kuibiwa mchana kweupe.
Alibembeleza yaishe nilipomwambia ‘kama kweli huu ndio Muungano tunaojivunia ninasikitika sana’.
Aliniruhusu kuondoka na pasi yangu baada ya kuelewa mimi ni kiumbe na sio miongoni mwa waliokuwa tayari kupata haki kwa kulipa kitu kidogo.
Kwa kweli usumbufu anaopata mtu anayesafiri kutoka Zanzibar kifika bandari ya Dar es Salaam ni mkubwa kuliko anayevuka mpaka wa Tanzania kwenda Kenya.
Suala hili limelalamikiwa sana hata ndani ya Bunge la Muungano na katika Baraza la Wawakilishi na siku zote wananchi hupewa ahadi ya kushughulikiwa na kutatuliwa, lakini badala yake usumbufu unazidi kila kukicha na kuzusha hasira juu ya Muungano na hasa mwenendo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wengi hatukushangaa kusikia Wawakilishi wakitaka ofisi za TRA zilipo Zanzibar zifungwe na watumishi wake wafunge virago kurudi Bara.
Baada ya hapo kila upande uwe na mfumo wake wa ushuru kama vile Bara na Visiwani hazikushirikiana kuunda kitu kinachoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivi karibuni wakurugenzi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) waliwataka wafanyabiashara wavumilie matatizo ya kulipa kodi mara mbili kwa vile suala hili linashughulikiwa.
Nilicheka sana baada ya kupitia kumbukumbu zangu na kuona malalamiko haya yamesikika kwa miaka mingi na siku zote jawabu lake ni “pole mwanangu”
na kufuatiwa na ahadi ya kupunguza maumivu.
Sasa watu wamechoka na ahadi za aina hii ambazo ni sawa na zile ambazo kuku humpa kifaranga chake anapotaka kunyonya.
Sijui na sifahamu ni utaalamu wa aina gani hutumiwa na TRA katika mpangilio wake wa kutoza kodi.
Ninachokiona ni vurugu. Mara nyingine utawakuta maofisa watatu au wanne wa TRA wanamuuliza mfanyabiashara masuala wa kiduka kidogo.
Kabla ya huyo jamaa hajajibu maofisa hao humtwanga masuala mengine na hata kupewa vitisho vya duka kufungwa. Ni mateso yasiyoelezeka.
Kichekesho kikubwa nilikipata katika kipindi cha TRA kilichotolewa katika runinga hivi karibuni. Ofisa mmoja mwandamizi alikiri kuwa wamegundua utaratibu wao wa kumtoza kodi ya mapato, mtu anayetaka kupatiwa leseni ya kufanya biashara ya kufungua duka sio sahihi.
Nilitarajia maelezo ziada. Kwanza kueleza nini kiliwafanya wawatoze watu kodi ya mapato hata kabla ya kufungua duka wala kununua bidhaa anazotaka kuuza.
Walichokuwa wakifanya TRA ni sawa na kumnunulia mwanamke nepi ya mtoto wakati hata hajabeba mimba.
Jingine la kiungwana ambao ofisa huyu angefanya, lakini aonekana hakuwa tayari, ni kuwaomba radhi watu waliodhulumiwa kwa kulazimishwa kulipa kodi ya mapato kabla ya mauzo.
Hapana ubishi kwamba malipo ya kodi ni wajibu wa kila mtu lakini inakuwaje hata umtoze mtu kodi ya mapato wakati hakuna kitu alichokiuza au kukipata?
Huwakosea Wazanzibari walipoeleza mfumo huu wa kodi kama ni wizi usiokuwa na mushkeli.
Wakati umefika kwa Serikali za Muungao na Zanzibar kuitafakari hali hii ambayo inapelekea baadhi ya watu kutoa kauli ambazo hazisaidii kuimasha muungano wetu.

No comments:

Post a Comment