Wednesday, March 7

Chadema, ACT wahaha madiwani wao kuhamia CCM


Wakati katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akianza ziara yake mkoani Kigoma, viongozi wa vyama vya ACT - Wazalendo na Chadema wamesema watakuwa tayari kuwalinda madiwani na viongozi wao wasitimkie CCM.
Kwa sasa ACT ina madiwani 19, Chadema mmoja na CCM wanao wanane. Vyama hivyo vya upinzani mkoani hapa vimeamua kujihami kutokana na wimbi la madiwani wa upinzani kujitoa katika vyama vyao na kuhamia CCM wakidai kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Naomi Kapambala amesema wakati wa ziara ya Polepole iliyoanza juzi wanatarajia kuvuna wanachama wapya kutoka vyama vya upinzani hasa Chadema na ACT vyenye wanachama na wafuasi wengi mkoani hapa. Licha ya kutowataja kwa majina, alisema kuna baadhi ya madiwani wameahidi kuachana na vyama vyao ili wajiunge na CCM kutokana na chama hicho kutekeleza ilani yake ya uchaguzi vizuri na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Wakizungumza na Mwananchi mjini Kigoma, viongozi wa vyama hivyo vya upinzani walisema wamepokea taarifa za kuwepo mikakati ya baadhi ya madiwani na viongozi wa vyama vyao kuhamia CCM, jambo lililowafanya kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na tishio hilo. Katibu wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Shabani Madede alisema alipata taarifa juu ya kadi za chama hicho kununuliwa kwa wingi katika Wilaya ya Uvinza kiasi kwamba baadhi ya matawi yameishiwa.
“Kadi zetu (Chadema) zinauzwa Sh1,500 lakini nimeelezwa kuwa kuna watu wanapitapita huko vijijini kwenye Wilaya ya Uvinza na kununua kadi kwa Sh3,000 hadi Sh5,000. Jambo hili lilinishangaza na nimetoa maelekezo kwa makatibu wote wa matawi, kata na majimbo kusitisha kuuza kadi,”alisema Madede.
Alisema kuna watu katika vyama vya siasa wamegeuza biashara kwa kununua wanachama kutoka vyama vingine, jambo linalodumaza na kudhoofisha demokrasia katika ushindani wa kisiasa.
“Tumejiandaa vya kutosha kulinda madiwani, viongozi na wanachama wetu kuhamia CCM, lakini inawezekana wachache wakadanganywa kwa kununuliwa na hivyo kujiunga CCM. Ikitokea tukasikia kuna waliohamia huko watakuwa ni wanachama hewa, bila shaka ndio hizo kadi zinazonunuliwa kwa bei kubwa,” alisema.
Katibu wa ACT Jimbo la Kigoma mjini, Azizi Ally alikiri kuwepo mikakati ya baadhi ya madiwani wa chama hicho kujiunga CCM. Hata hivyo, alisema hatarajii kuona hilo likifanyika.
Alisema wametumia nguvu na gharama kubwa kukijenga chama hicho tangu mwaka 2014 na kwamba, madiwani wote walio nao waliwapigania kushinda kwenye kata zao. Tayari madiwani hao wanadaiwa kula kiapo cha uaminifu kwa chama chao na kuahidi kuwatumikia wananchi wa Kigoma mjini kutokana na chama chao kuongoza manispaa, kazi ambayo hawajaitekeleza kutokana na kuwepo ahadi zinazoendelea kutekelezwa.
Akimnadi aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel, Januari 27, naibu katibu mkuu wa chama hicho, Rodrick Mpogolo alisema viongozi wa upinzani wanajiunga na CCM baada ya kubaini ajenda ya kuwahudumia wananchi ipo katika chama hicho.

No comments:

Post a Comment