Serikali ya Tanzania imesema kuwa haitatoa ruzuku yoyote kwa benki zitakazoshindwa kujiendesha zenyewe.
Badala yake imezitaka benki changa kuungana na benki nyingine zenye mitaji mikubwa ili ziweze kuendelea kuboresha hisa zao.
Wakati akizindua tawi la benki ya CRDB Wilayani Chato, Mkoani Geita, Ijumaa Rais Magufuli, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza mchakato wa kuzifuatilia benki zote ambazo zinasuasua na zilizokuwa na mitaji ya Serikali kuzichukua.
Amesema bora zibaki benki chache ambazo zinauwezo wa kutoa huduma kwa wananchi masikini na kusisitiza zitakazoshindwa kujiendesha zenyewe basi nazo zifungiwe.
Zaidi aliipongeza BoT kwa uamuzi wake wa kuzifungia benki zaidi ya tano na kutoa muda wa matazamio kwa nyingine tatu.
Akiizungumzia benki ya CRDB, Rais Magufuli, aliipongeza kwa kuwa miongoni mwa benki 50 zinazofanya vizuri kwa sasa zikitoa huduma na kuwafikia wananchi katika kila eneo kwa kuwa na matawi zaidi ya 250 nchini huku ikitoa fursa ya ajira kwa Watanzania zaidi ya 4,000.
Kutokana na hilo, Rais Magufuli alieleza kuguswa na utendaji kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, hivyo kumhakikishia ajira serikalini kwa asilimia 100 pindi atakapostaafu utumishi wake ndani ya benki hiyo.
No comments:
Post a Comment