Saturday, March 10

Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Odinga, waahidi kuwaunganisha Wakenya

Raila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa KenyaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionRaila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo Raila Odinga katika afisi yake Jumba la Harambee, Nairobi.
Wawili hao wamekubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa rasmi karibuni
Balozi Martin Kimani ataongoza kuundwa kwa mpango huo upande wa Rais Kenyatta naye mshauri wa Bw Odinga Paul Mwangi atawakilisha Bw Odinga, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Bw Kenyatta na Bw Odinga baada ya mkutano huo.
Mkutano huo ulifanyika muda mfupi kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.
Bw Tillerson, akihutubu baadaye amewasifu wawili hao kwa kukutana.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake kuhusu kukandamizwa kwa kidemokrasia nchini Kenya, akitaja wka mfano kufungiwa kwa baadhi ya vituo vya runinga nchini humo hivi majuzi.
Marekani imekuwa ikihimiza kufanyika kwa mazungumzo na mashauriano kutatua mzozo wa kisiasa uliokumba taifa hilo baada ya uchaguzi uliojaa utata mwaka jana.
Naibu Rais William Ruto ameonekana kufurahishwa na mkutano huo.
Bw Mungai Kihanya naye amelinganisha mkutano wao wa leo na tangazo kwamba Rais wa Marekani Donald Trump atakutana na kiongozi wa Korea Kaskazini hivi karibuni.
Bw Odinga alitangulia kuhutubia taifa moja kwa moja na baadaye Bw Kenyatta akatoa hotuba yake.
Bw Kenyatta amesema wamekubaliana na Bw Odinga kwamba taifa la Kenya ni muhimu kuliko mtu binafsi na kwamba lazima viongozi washirikiane.
Rais huyo amesema siku za usoni za Kenya haziwezi kuongozwa na uchaguzi ujao bali "uthabiti wa taifa."
"Demokrasia si mwisho wa kila kitu. Ni shughuli na nia ya wananchi lazima iongoze."
"Tumekubaliana tutaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna araia anayehisi ametengwa."
"Huu ni mwanzo mpya kwa taifa letu."
"Tunaweza kutofautiana lakini kusalia tukiwa tumeungana kama Wakenya."
Raila na Uhuru
Bw Odinga amesema kwa muda mrefu Kenya imeangazia kubadilisha taasisi na miaka saba iliyopita katiba mpya ilianza kutekelezwa.
"Sasa lazima tuwe na ujasiri wa kukubali kwamba hilo halijafanikiwa. Bado hatujabadilisha mengine," amesema Bw Odinga.
"Ndugu yangu na mimi tumekutana pamoja leo na kusema yamefikia kikomo. Tumekataa kuwa watu ambao chini yake Kenya imekuwa taifa lililofeli."
Bw Tillerson atawasili nchini Kenya baadaye leoHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionBw Tillerson atawasili nchini Kenya baadaye leo
Bw Odinga amesema wamekubaliana kufanikisha mabadiliko yatakayofanikiwa mageuzi nchini humo, na pia kukomesha kulaumiana.
Amewataka Wakenya waunge mkono mpango wa viongozi hao wawili.
"Tumesafiri mbali sana kiasi kwamba hatuwezi kurudi tena bandarini. Isitoshe, hatuwezi kufika tunakoenda bila kufanya mabadiliko la sivyo tutazama baharini," amesema Bw Odinga.
"Tumekuja pamoja na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha hapa na sisi. Tutembee pamoja," amesema Bw Odinga.

Matukio makuu mzozo wa kisiasa Kenya

  • 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
  • 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
  • 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
  • 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya
  • 9 Machi, Bw Kenyatta akutana na Bw Odinga katika afisi ya rais Jumba la Harambee, wawili hao waahidi kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.

Kushinikiza mageuzi

Bw Odinga alisusia kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika 26 Oktoba mwaka jana akishinikiza mageuzi yafanywe kwanza katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Uchaguzi huo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ikisema ulikuwa na kasoro nyingi.
Mahakama hiyo ilikuwa inatoa uamuzi katika kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bw Odinga kupinga matokeo hayo.
Bw Kenyatta alishinda uchaguzi huo wa marudio kwa kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Idadi ya waliojitokeza ilikuwa ni asilimia 38.84 ya waliokuwa wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo.
Uchaguzi ulitatizika sana katika maeneo yenye wafuasi wengi wa upinzani. Katika majimbo manne magharibi mwa Kenya ambayo ni ngome ya Bw Odinga, uchaguzi uliahirishwa kwa siku kadha na baadaye haukufanyika.

No comments:

Post a Comment