Saturday, March 10

Mwandishi wa Uganda ajishindia tuzo kubwa kabisa duniani ya uandishi

Jennifer Nansubuga MakumbiHaki miliki ya pichaMARK RUSHER
Image captionMwandishi wa vitabu ,Jennifer Nansubuga Makumbi
Wachapishaji wa vitabu nchini Uingereza walikataa kuchapisha riwaya za mwandishi wa Uganda ambaye makazi yake ni Manchester Uingereza lakini sasa ameweza kujishindia moja ya tuzo kubwa kabisa duniani ya uandishi.
Jennifer Nansubuga Makumbi ni mwandishi ambaye alitoka nchini Uganda miaka 17 iliyopita na kuhamia Uingereza .
Makumbi ameweza kujishindia tuzo za Windham Campbell yenye thamani ya dola 165,000 kutoka kutoka chuo kikuu cha Yale kilichopo nchini Marekani.
Makumbi amesema ushindi huu umemshangaza ingawa huwa anafanya kila kitu muhimu katika uandishi wake.Mwandishi huyo anasema kiasi hicho cha fedha ni muda mrefu umepita hajawahi kukishika.
Fedha iliyotolewa katika tuzo hii ni mara mbili ya kiasi cha fedha kinachotolewa kwa mshindi wa Booker Prize na waandaaji wanasema tuzo hii ni kubwa zaidi katika uandishi wa vitabu baada ya Noble Prize.
Makumbi ni mmoja kati ya washindi wanane waliopokea tuzo za Windham Campbell kwa mwaka huu katika uandishi wa riwaya za kubuni ,uhalisia ,maigizo na ushairi na yeye ni mshindi pekee aliyechapisha kazi moja kamili ya muda mrefu.
Waandishi wengine kutoka Uingereza waliokuwa kwenye orodha wote wakiwa wanaandika simulizi zenye uhalisia walikuwa ni Sarah Bakewell na Olivia Laing.
Tuzo hizo zilizoanzishwa na Donald Windham na kubeba jina lake pamoja na mshirika wake Sandy M Campbell na tuzo za kwanza zilianza kutolewa mwaka 2013 na kuwapa waandishi fursa ya kuzingatia kazi zao wakiwa huru bila changamoto za kifedha.
Makumbi anasema taarifa hii ya kupata tuzo hakuitarajia kwa kuwa inaandaliwa na wamarekani na kwa kawaida huwa wanapata vitabu vingi, "Ninashangaa kuwa miongoni mwa washindi"alisema.
MakumbiHaki miliki ya pichaIMAGE COPYRIGHTONEWORLD PUBLICATIONS
Image captionKitabu cha Makumbi
Toleo la riwaya yake ya kwanza ,Makumbi aliichapisha nchini Kenya miaka minne baada ya wachapishaji wa Uingereza kukataa kuchapisha kitabu chake cha "Too African"na baadae januari mwaka huu kitabu hicho kilizinduliwa nchini Uingereza.
Mwandishi alisema wachapishaji na wasomaji wa Uingereza wanapenda kusoma vitu ambavyo vinaendana na tamaduni zao za ulaya au ambazo wamezizoea hata kama wanasoma simulizi kuhusu Afrika.
Lakini amekielezea kitabu cha" Kintu" kuwa kinazungumzia Uafrika halisi.
Kitabu hiki kimeangazia hadithi ya simulizi za famila moja ya Uganda ambayo waliamini kuwa walilaaniwa kwa zaidi ya miaka 250.
Mwandishi huyo anasema namna ambavyo ameandika kitabu chake wasomaji walikuwa hawajauzoea ila sasa anaamini wataanza kumuelewa.
Kama ninataka kuitambulisha Afrika lazima niieleze katika mrengo wa kiafrika badala ya kuwaambia vitu ambavyo wanatarajia kuwa wanavijua .

No comments:

Post a Comment