Saturday, March 10

Wakimbizi wa Burundi waikimbia DRC na kuingia Rwanda

Kambi ya Nyarushishi ambapo wakimbizi hao wamekimbilia
Image captionKambi ya Nyarushishi ambapo wakimbizi hao wamekimbilia
Wakimbizi zaidi ya elfu 2500 wa Burundi waliokuwa katika kambi ya Kamanyola Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo tangu Jumatano wamekimbilia nchini Rwanda kwa kile ambacho wanasema ni kuhofia usalama wao.
Wanapinga utaratibu wa kisasa unaotumiwa wa kusajili wakimbizi kwa kunasa alama zao za vidole.
Wakimbizi hao wanasema hawatakubali kuishi katika nchi yoyote inayotumia mfumo huo wa usajili kwamba ni kinyume na imani yao.
Rwanda pia hutumia mfumo huo na tayari ilikuwa imeanza kuwasajili wakibizi wa Burundi waliotangulia kuhamia nchini humo.
Mwandishi wa BBC Yves Bucyana amewatembelea katika kambi ya Nyarushishi magharibi mwa nchi hiyo ambako wamepokelewa kwa muda.
Wakimbizi wapatao elfu 2,553 ndio tayari wameletwa katika kambi hii ninakosimama hivi sasa.
Ni kambi iliyojengwa kwa nyumba za kisasa kiasi kwamba wanapata sehemu nzuri ya kujikinga mvua au jua.
Tangu asubuhi nilipofika hapa nimeshuhudia vikao ambavyo bado vinaendelea baina ya shirika la umoja wa mataifa la wakimbizi UNHCR na wawakilishi wa wizara ya Rwanda inayohusika na maswala ya wakimbizi.
Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria vikao hivyo wala kuwasogelea wakimbizi ndani ya kambi,lakini nje ya kambi tayari nilikuwa nimezungumza na mmoja wao mzee Charles Ntagwarara kuhusu sababu hasa zilizowafanya kukimbilia katika nchi ya tatu:
"Monusco na serikali ya Congo walitushinikiza kukubali tusajiliwe kwa mtindo wa kisasa wa kunasa picha na ishara za vidole ili tupate kitambulisho rasmi kwamba sisi ni wakimbizi.
Hii ni kinyume na imani yetu kwani ni miaka 30 tangu Bikra Maria kutangaza kwamba shetani atapitia katika mambo mengi miongoni mwake ni mtindo huo.ni shetani ambaye ameingilia katika mambo hayo ya kisasa.''
Wakimbizi
Rwanda ni nchi ambayo tayari inatumia mfumo huu wa kielectroniki kuwasajili wakimbizi,ikiwa mwezi uliopita lilianza zozezi la kuwasajili wakimbizi wa Burundi ambao wamemaliza zaidi ya miaka 2 wakiwa nchini hapa.Nimetaka kujua watafanyaje kwa sababu wanaangukia katika nchi ambayo tayari inatumia mfumo wa usajili ambao hawataki?Mzee Charles Ntagwarara tena:
"Sisi hatuwezi kukubali mambo haya. Dunia ina nchi zaidi ya 200.si unaona kwamba tuko nchini Rwanda? Sisi tunatafuta nchi ambayo itakubali kutupokea pasipo kutusajili kwa kutumia utaratibu huo. Nchi ambayo itatwambia kwamba haitanasa ishara za vidole vyetu tutaishi humo.hata vyakula au madawa ambayo hayamo katika imani zetu hatuwezi."
Muda niliokaa hapa kambini nimeambiwa pia kwamba wakimbizi hawa hutumia baadhi ya vyakula vyao maalumu ambao sikuweza kujua; kadhalika kutokana na imani yao siyo kila dawa wanayokubali nikiambiwa kwamba wanao wahudumu wao wa afya wanaoshirikiana na watu wa msalaba mwekundu waliopo hapa na mashirika mengine ya misaada.Kilicho wazi hadi kufikia sasa wakati tunasubiri msimamo wa serikali ni kwamba wao bado wanachukuliwa kuwa ni wahamiaji wanaotafuta ukimbizi nchini Rwanda.

No comments:

Post a Comment