Monday, March 12

Ndege yaanguka, abiria wahofiwa kufa


Kathmandu, Nepal. Ndege ya shirika la ndege la US-Bangla iliyokuwa imebeba abiria 67 na wafanyakazi wanne imeanguka na kuwaka moto ilipokuwa inataka kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kathmandu.
Maofisa wamesema wamefanikiwa kutoa miili kadhaa na majeruhi kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo ya Bangladesh. Ndege hiyo ilikuwa inatokea Dhaka, Bangladesh ilipoanguka kwenye uwanja wa mpira ambao upo karibu na uwanja wa ndege.
Msemaji wa serikali hakuweza kutaja idadi lakini alisema waliokufa na majeruhi wameondolewa kwenye mabaki ya ndege hiyo. Ofisa mwingine aliliambia shirika la habari la AFP kwamba watu 20 walijeruhiwa na walipelekwa hospitalini.
Miali ya moshi mzito na moto iliweza kuonekana kutoka kwenye uwanja wa mpira ambako ndege iliangukia mashariki mwa sehemu ya kukimbilia ndege katika uwanja pekee wa kimataifa mjini Kathmandu.
"Polisi na jeshi wanajaribu kukatakata mabaki ya ndege katika juhudi za kuokoa wengine," alisema msemaji wa uwanja wa ndege Prem Nath Thakur.
Picha zilizorushwa kwenye mtandao wa Facebook zinaonyesha miali ya moshi mzito ikipanda juu nyuma ya sehemeu ya ndege kukimbilia, ambako ndege nyingine ilikuwa imesimama.

No comments:

Post a Comment